Na Atley Kuni, WAF-Dodoma
Wakufunzi wa Chuo cha Afya Mvumi wametakiwa kuzingatia mafunzo maalum yanayotolewa na wizara ya afya kuhusu afya ya uzazi ili waweze kuendana na mahitaji ya sasa, hatua itakayo wezesha kuokoa uhai wa mama na mtoto.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Mafunzo hayo kwa kutoka Wizara ya Afya Notgera Ngaponda, leo Julai 13, 2026 wakati akifungua rasmi mafunzo ya wakufunzi wa afya ya uzazi, mama na mtoto kwa Mkoa wa Dodoma yanayofanyika katika Chuo cha Afya Mvumi, yakihusisha wakufunzi 12 wa chuo hicho
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Ngaponda amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuweka kipaumbele katika ujenzi wa uwezo wa rasilimali watu ili kuhakikisha huduma za afya zinazotolewa nchini zinakuwa bora, salama na zenye kuzingatia Utu , heshima na viwango kwa mujibu wa miongozo ya kitaifa na kimataifa.

”Ubora wa huduma za afya huanza na ubora wa mafunzo yanayotolewa kwa wataalamu wa afya, hivyo wakufunzi wana nafasi ya kipekee katika kuzalisha wahitimu wenye maarifa, ujuzi na maadili yatakayowezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi” amesema Ngaponda.
Ngaponda amewataka washiriki kutumia mafunzo hayo kama fursa ya kuongeza maarifa, kujifunza mbinu mpya za ufundishaji na kubadilishana uzoefu utakaochangia kuimarisha elimu ya afya ya uzazi, mama na mtoto katika taasisi yao.
Aidha, amewahimiza washiriki kushiriki kikamilifu katika mijadala na kazi za vitendo zitakazowasilishwa wakati wa mafunzo, akisisitiza kuwa maarifa watakayoyapata yanapaswa kuwafikia watumishi wengine wa afya kupitia mafunzo endelevu katika maeneo yao ya kazi.
Katika hatua nyingine Notgera amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika maendeleo ya sekta ya afya kupitia mafunzo ya mara kwa mara kwa wakufunzi na watumishi wa afya, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha ubora wa huduma za afya na kuongeza ustawi wa wananchi.

Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka, yakitarajiwa kuwaongezea uwezo wa kitaaluma na kuwawezesha kutumia mbinu za kisasa za kufundisha na kusimamia utoaji wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuendelea kwa siku mbili katika Chuo cha Afya Mvumi, Mkoa wa Dodoma, huku yakilenga kuimarisha uwezo wa wakufunzi ili kuongeza ubora wa elimu ya afya na kuchangia juhudi za Serikali za kuboresha huduma za afya kwa wananchi nchini.
Mafunzo kama hayo yanatolewa kwenye vyuo 47 vya kati na vya elimu ya juu nchi nzima vikiwahusisha wakufunzi 450.

































