Wananchi wanaoishi na VVU jijini Dar es Salaam wanahitaji kuendelea kupata huduma za upimaji, matibabu na uangalizi bila kukatizwa, huku Serikali na wadau wa afya wakijipanga kuimarisha mifumo ya utoaji huduma hizo katika kipindi ambacho ufadhili kutoka nje unakabiliwa na mabadiliko.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, katika mkutano wa wadau wa huduma za VVU na UKIMWI uliofanyika jijini Dar es Salaam Oktoba 8, 2026.

Mapunda amesema ushirikiano endelevu kati ya Serikali, watoa huduma za afya, washirika wa maendeleo na jamii ni muhimu katika kulinda mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya VVU na kuhakikisha wananchi wanaohitaji huduma hizo wanazipata kwa wakati.

Amesema ongezeko la idadi ya watu jijini Dar es Salaam pamoja na mwingiliano mkubwa wa watu kutoka maeneo mbalimbali vinaongeza changamoto katika kudhibiti maambukizi mapya na kupanua upatikanaji wa huduma za afya. Hivyo, juhudi zaidi zinahitajika katika kuimarisha kinga, kutoa elimu kwa umma na kuwahamasisha wananchi kupima na kupata matibabu.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutumia takwimu sahihi katika kupanga huduma za afya ili kubaini mahitaji ya wananchi, kuelekeza rasilimali kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa na kuboresha utoaji wa huduma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Amref Health Africa Tanzania, Dk. Florence Temu, amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya na wadau wengine kuhakikisha huduma za VVU zinaendelea kutolewa kwa ubora unaotakiwa.

Amesema kipaumbele ni kujenga juu ya mafanikio yaliyopatikana kwa zaidi ya miongo miwili, huku ikiimarishwa uwezo wa ndani na umiliki wa Serikali katika kusimamia mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.

Kupitia Mradi wa Afya Thabiti unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani, Amref inaunga mkono utoaji wa huduma za kinga, matunzo na matibabu ya VVU katika vituo vya afya na ngazi ya jamii.

Huduma hizo zinajumuisha kuwabaini watu wanaoishi na VVU na kuwaunganisha na matibabu, kuimarisha mifumo ya maabara, kufuatilia utekelezaji wa programu na kuboresha ubora wa takwimu za afya.

Hatua hizo zinalenga kuhakikisha huduma zinaendelea kupatikana, huku watoa huduma za afya wakipata uwezo wa kubaini mapungufu katika utoaji wa huduma, kufuatilia maendeleo ya wagonjwa na kupanga matumizi ya rasilimali kwa ufanisi zaidi.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Programu wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vya Marekani (CDC) nchini Tanzania, Dk. George Mgomella, amesema ushirikiano imara kati ya Serikali na taasisi zinazotekeleza programu za afya ni muhimu katika kuhakikisha huduma zinaendelea na kuimarisha mapambano ya nchi dhidi ya VVU.

Amesema mabadiliko ya taasisi inayotekeleza programu hizo yanaweza kuwa fursa ya kuimarisha ushirikiano na kujenga juu ya mafanikio yaliyokwisha kupatikana. Ameongeza kuwa CDC ya Marekani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania pamoja na wadau wake kusaidia upatikanaji wa huduma bora na endelevu za VVU.

Amref ilianza kutekeleza huduma za VVU jijini Dar es Salaam Januari 2026, baada ya kukabidhiwa majukumu hayo kutoka Shirika la Management and Development for Health (MDH), lililokuwa likiunga mkono utoaji wa huduma hizo kwa takribani miongo miwili.

Mabadiliko hayo yamehusisha mamlaka za Serikali, watoa huduma za afya na washirika wa maendeleo katika kuoanisha vipaumbele vya programu, kuweka wazi majukumu ya kila mdau na kuimarisha uratibu ili kuhakikisha huduma zinaendelea kuwafikia wananchi.

Katika mkutano huo, wadau pia wamejadili mafanikio yaliyopatikana, changamoto za utekelezaji wa programu na hatua zinazoweza kuchukuliwa kuboresha huduma za VVU, UKIMWI na kifua kikuu jijini Dar es Salaam.

Juhudi hizo zinaunga mkono azma ya Tanzania kufikia malengo ya kimataifa ya 95-95-95. Malengo hayo yanalenga kuhakikisha asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali zao za maambukizi, asilimia 95 ya waliobainika kuwa na VVU wanapata matibabu, na asilimia 95 ya wanaopata matibabu wanafikia kiwango cha virusi mwilini kisichoweza kugundulika kwa vipimo husika.

Mafanikio katika maeneo hayo ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kutokomeza UKIMWI kama tishio kwa afya ya umma ifikapo mwaka 2030.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *