Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza kutoa mafunzo kwa taasisi za umma kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi, yakilenga kuongeza uelewa na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya kikodi.

Mafunzo hayo yamefunguliwa Septemba 24, 2026, jijini Dodoma na Naibu Kamishna wa Oparesheni wa Idara ya Walipakodi Wakubwa, Eva Raphael.

Akifungua mafunzo hayo, Eva amesema uelewa wa mabadiliko ya sheria za kodi ni muhimu kwa taasisi za umma ili ziweze kutekeleza wajibu wao kwa usahihi, kwa wakati na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Washiriki pia wamepatiwa mafunzo kuhusu matumizi ya mfumo wa IDRAS na Mfumo wa Ulipaji Serikalini (MUSE), yakilenga kuongeza ufanisi katika uwasilishaji na usimamizi wa taarifa na miamala inayohusiana na kodi.

Katika hatua nyingine, TRA imetoa vyeti kwa taasisi zilizofanya vizuri katika kutekeleza wajibu wao wa kikodi, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha uzingatiaji wa sheria na taratibu za kodi.

TRA imesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano na taasisi za umma, kuongeza uelewa wa masuala ya kodi na matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali katika utekelezaji wa majukumu ya kikodi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *