• June 27, 2024
  • Mwandishi Wetu
  • 0

Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, imetakiwa kubuni vyanzo vipya vya mapato ya ndani, ili kupata fedha zitakazosaidia kutekeleza na kuibua miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi.

Agizo hilo limetolewa leo Julai 9, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, alipokuwa akitoa salamu za mkoa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani, kilichokuwa na ajenda ya kupokea na kujadili hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo halmashauri hiyo imepata hati safi.

Mhita amesema kuwa, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fedha nyingi mkoani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi, na kwamba kufuatia hatua hiyo, amezitaka halmashauri kuongeza ubunifu katika kukusanya wa mapato, ili kuonyesha dhamira ya dhati ya kumuunga mkono Rais katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Aidha, ameipongeza halmashauri hiyo kwa kufanikiwa kupata hati safi inayoridhisha, akibainisha kuwa hiyo ni ishara ya usimamizi mzuri wa fedha za umma zinazoelekezwa kwenye miradi.

Awali Mwekahazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Shimi Emmanuel, akisoma taarifa ya CAG, amesema kuwa halmashauri hiyo ilikuwa na jumla ya hoja 29. Kati ya hizo hoja 10 zimefungwa kikamilifu, huku hoja 19 zilizosalia zikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Kwa upande wake mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali CAG Mkoa wa Shinyanga Yusuph Marwe, ametoa ushauri kwa menejimenti ya Halmashauri hiyo kwamba katika ufutaji wa hoja, miradi ya muda mrefu ipewe kipaumbele ili ikamilike na kuhakikiwa na CAG na kufungwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *