Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imetangaza kushiriki Maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kitaifa 2026 yatakayofanyika kuanzia Agosti 1 hadi 8 katika viwanja vya Dk. John Malecela, Dodoma, ikiwa na lengo la kuwaunganisha wadau wa sekta ya nafaka na mazao mchanganyiko na fursa za masoko, biashara, teknolojia na uongezaji thamani.

Ushiriki huo unaendana na kaulimbiu ya Nanenane 2026, “Tambua Soko; Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050,” kwa kuhamasisha uzalishaji unaozingatia mahitaji ya soko, ubora wa mazao, biashara rasmi na matumizi ya teknolojia ili kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania.

Katika maonesho hayo, banda la COPRA litatoa elimu na ushauri wa kitaalamu kuhusu masoko ya ndani na kimataifa, viwango vya ubora, uongezaji thamani, mifumo rasmi ya biashara pamoja na huduma za kidijitali kupitia mfumo wa COPRAMIS.

Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Madeje Mlola, amesema lengo ni kuhakikisha wakulima, wafanyabiashara, wasindikaji, wawekezaji na vijana wanapata taarifa sahihi zitakazowawezesha kufanya maamuzi bora katika uzalishaji na biashara ya nafaka.

“Tunataka kila anayefika banda la COPRA aondoke akiwa na uelewa wa uzalishaji wenye tija, ubora wa mazao, masoko na fursa zinazoweza kuongeza thamani ya mazao yake. Pia tunahamasisha matumizi na uongezaji thamani wa mazao yanayozalishwa nchini ili kuimarisha soko la ndani,” amesema Mlola.

Miongoni mwa shughuli maalumu zitakazofanyika ni Warsha ya Zao la Mahindi itakayofanyika Agosti 5, 2026, ikiwakutanisha wadau kujadili uzalishaji, masoko, uwekezaji, mitaji na uongezaji thamani wa zao hilo.

Aidha, Agosti 7, 2026 kutafanyika Digital Agribusiness Influencers Day, itakayowakutanisha watengeneza maudhui ya biashara ya mazao mtandaoni na COPRA kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya majukwaa ya kidijitali katika kutangaza masoko, teknolojia na fursa za biashara.

COPRA pia itakuwa na eneo maalumu la vyakula vya lishe vinavyotokana na mazao yanayosimamiwa na mamlaka hiyo, likiwemo choroko, dengu na mbaazi, kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya mazao ya ndani na kufungua fursa zaidi za uongezaji thamani na biashara kwa wakulima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *