Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Mama Fatma Karume, aliyefariki dunia Jumatatu, Septemba 21, 2026.
Mama Fatma alikuwa mjane wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Katika salamu zake, Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mama Fatma, akieleza kuwa kifo chake ni pengo kwa familia na Taifa kwa ujumla.
“Mama Fatma Karume alikuwa sehemu muhimu ya historia ya Zanzibar, hususan katika vipindi vya harakati za kupigania uhuru, Mapinduzi ya Zanzibar na kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Rais Samia.
Amesema Taifa litaendelea kukumbuka, kuenzi na kuheshimu mchango wa Mama Fatma katika kuhifadhi kumbukumbu na urithi wa Taifa, pamoja na kuchochea maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Rais Samia pia ametoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, familia ya Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, ndugu, jamaa na marafiki na wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote kufuatia msiba huo.





























































































































































































































































