Jeshi la Polisi Tanzania limeendelea kuwawezesha askari kupitia mafunzo ndani na nje ya nchi, huku kundi la maafisa, wakaguzi na askari likielekea Indonesia kwa mafunzo yatakayolenga kuongeza ujuzi katika utendaji wa kazi.
Akiwaaga washiriki hao kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camillus Wambura, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA), DCP Dkt. Lazaro Mambosasa, amewataka kutumia maarifa watakayopata kuboresha huduma kwa wananchi.

Amesema washiriki wanapaswa kuzingatia nidhamu, weledi na maadili ya Jeshi la Polisi wakati wote wa mafunzo na kuhakikisha wanaliwakilisha vyema taifa.
Mambosasa amesema mafunzo hayo yatajikita katika maeneo ya uongozi na maendeleo ya kitaaluma, ulinzi shirikishi, teknolojia zinazoibukia ikiwemo Akili Bandia (AI), uchunguzi wa jinai, matukio makubwa pamoja na ubunifu katika utendaji.
Amesema ujuzi huo unatarajiwa kusaidia kuboresha utendaji wa kila siku wa Jeshi la Polisi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mafunzo hayo ya International Association of Women Police (IAWP) yanashirikisha zaidi ya nchi 64.































































































































































































































































