Baadhi ya wananchi wamesema wamevutiwa na namna ambavyo Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) wanavyotoa miongozo na fursa zinazoweza kupatikana katika sekta ndogo ya Mafuta na Gesi asilia nchini.
Wakizungumza katika Maonesho ya Nanenane jijini Dodoma, kwenye banda la PURA, wananchi hao wamesema kuwa kupitia elimu waliyoipata wamefahamu ni kwa namna gani wawekezaji wanapatikana kutekeleza miradi hiyo.
Wamesema kuwa kufuatia miongozo ambayo imewekwa na PURA wananchi wanapata taarifa juu ya namna ya kushiriki katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli kwa uwazi na kwa wakati.

Kwa upande wake Mjiolojia Kutoka PURA, Desmond Risso amefafanua kwa wananchi hao kuwa pamoja na mambo mengine, pia Mamlaka hiyo imeweka mfumo kwa ajili ya kuwezesha kuwatambua watoa huduma na wafanyabiashara wa kitanzania wenye uwezo kushiriki katika miradi inayotekelezwa.
Risso amesema mfumo huo pia, unawakutanisha na kampuni za kimataifa zinazotekeleza miradi hiyo hapa nchini na kutambua fursa zilizopo.
Maonesho ya Nanenane yanaendelea katika viwanja vya Nzuguni Dodoma ambapo PURA inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli za utafutaji uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.






























































































































































































































































