📌Wananchi Wajitokeza kwa Wingi, Wampongeza kwa Uongozi wa Vitendo
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, ameongoza zoezi la usafi kwa vitendo katika Stendi Kuu ya Mabasi Kilosa, akishirikiana na wananchi, wafanyabiashara na watumishi wa serikali.
Shaka alionekana akiwa amevaa glavu, kubeba gunia na kutumia ufagio kuokota taka zilizokuwa katika eneo la stendi na soko, ikiwemo mifuko ya plastiki na uchafu uliokuwa umejaa katika mitaro.
Amesema viongozi wanapaswa kuwa mfano katika utekelezaji wa masuala ya usafi, akisisitiza kuwa stendi na soko ni sehemu muhimu ya taswira ya Wilaya ya Kilosa.
“Leo hatujaja kupiga picha. Tumeamua kutoka ofisini kuja mtaani kufanya usafi kwa vitendo, sio kwa maneno. Kiongozi lazima aongoze kwa mfano,” amesema.
Amesema usafi unapaswa kuendelea katika maeneo yote ya umma na majumbani, huku kila mwananchi akiwajibika katika kulinda mazingira.
Aidha, Shaka ameagiza Halmashauri kuhakikisha kila mfanyabiashara anakuwa na dumu la taka mbele ya eneo lake la biashara, akionya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaokaidi.
Zoezi hilo lilishirikisha mamia ya wananchi, wakiwemo mama ntilie, madereva wa bodaboda, watumishi wa serikali na maafisa wa vyombo vya ulinzi na usalama.






























































































































































































































































