• August 6, 2026
  • Mwandishi Wetu
  • 0


DODOMA:
 Wakurugenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) wameungana na watumishi wa Mfuko kutoa huduma kwa wanachama na wananchi wanaotembelea banda la PSSSF katika Maonesho ya Kilimo na Uvuvi (Nanenane) yanayoendelea kitaifa katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.

Hatua hiyo inaonyesha dhamira ya uongozi wa PSSSF ya kusogeza huduma karibu na wanachama na wananchi, sambamba na kuimarisha utoaji wa huduma kwa ufanisi na weledi.

Katika banda hilo, PSSSF inatoa elimu kuhusu hifadhi ya jamii, kuwaunganisha wanachama na wastaafu kwenye huduma za kidijitali kupitia PSSSF Kiganjani na PSSSF Portal, pamoja na kutoa taarifa kuhusu fursa za uwekezaji zinazopatikana kupitia miradi ya Mfuko.

Miradi hiyo ni pamoja na Kiwanda cha Bidhaa za Ngozi (KLICL) na Machinjio ya Kisasa ya Nguru Hills yaliyopo Wilaya ya Mvomero.

Wakurugenzi walioshiriki kutoa huduma Agosti 6, 2026 ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Paul Kijazi; Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Hilda Nkunna; na Mkurugenzi wa Manunuzi na Ugavi,  Jimmy Mbogela.

Awali, Agosti 5, 2026, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Eric Kato, naye alishiriki kutoa huduma kwa wanachama na wananchi waliotembelea banda hilo.

Sambamba na hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji, Bw. Hajj Moshi, aliongoza timu ya wataalamu wa PSSSF kutembelea mabanda mbalimbali ya waoneshaji kwa lengo la kutoa elimu kuhusu maboresho ya huduma za Mfuko na kupokea maoni kutoka kwa wanachama na wananchi.

Akizungumza kuhusu ushiriki huo, Meneja wa Uhusiano na Elimu kwa Wanachama wa PSSSF, Omega Ngole, amesema hatua ya wakurugenzi kushiriki moja kwa moja katika utoaji wa huduma inaonesha dhamira ya uongozi wa Mfuko ya kuwathamini wanachama na wananchi, huku ikiwapa motisha watumishi kuendelea kutoa huduma bora.

“Ushiriki wa wakurugenzi katika kuhudumia wanachama ni sehemu ya utamaduni wa PSSSF wa kusogeza huduma karibu na wananchi na kuhakikisha kila mteja anapata huduma bora kwa wakati,” amesema Ngole.

Ameongeza kuwa, mbali na maonesho ya kitaifa yanayoendelea jijini Dodoma, PSSSF pia inaendelea kutoa huduma katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika kanda nyingine nchini, zikiwemo Kanda ya Magharibi (Tabora), Kanda ya Ziwa Magharibi (Mwanza), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kanda ya Kusini (Lindi) pamoja na Zanzibar.

Kupitia ushiriki huo, PSSSF inaendelea kusogeza huduma karibu na wananchi, kuongeza uelewa kuhusu hifadhi ya jamii na kuwahamasisha wanachama kutumia huduma za kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za Mfuko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *