Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani imeishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Sh19.8 bilioni kupitia mradi wa TACTIC, unaolenga kuboresha miundombinu mbalimbali katika Manispaa hiyo.
Shukrani hizo zimetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dk. Nicas Mawazo, wakati akipokea na kuzindua magari mawili aina ya Ford Ranger yaliyotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Dk. Mawazo amesema mradi huo wenye thamani ya Sh19.8 bilioni unatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika uboreshaji wa miundombinu na kuongeza kasi ya maendeleo katika Manispaa ya Kibaha.
Amesema magari hayo ni sehemu ya makubaliano ya mkataba wa mradi wa TACTIC na yatatumika katika shughuli mbalimbali za utekelezaji na usimamizi wa miradi, huku baada ya kukamilika kwa matumizi yake yakirejeshwa katika Halmashauri kwa ajili ya shughuli nyingine.
“Katika miradi hii ya TACTIC tunakwenda kuitekeleza kwa ubora zaidi na Halmashauri ya Kibaha inaenda kuwa ya kwanza na mfano kwa Halmashauri nyingine katika utekelezaji na usimamizi wa miradi hii nchini,” amesema.
Dk. Mawazo amewataka wananchi wa Kibaha kujivunia na kutangaza maendeleo yanayofanywa na Serikali, akisema Manispaa hiyo inanufaika na utekelezaji wa dira ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema maendeleo yanayotekelezwa kwa kasi yanaifanya Kibaha kuwa na fursa ya kuwa Halmashauri ya mfano katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, Mrisho Mlela, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta miradi yenye fedha nyingi katika Manispaa hiyo.
Pia amewashukuru Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon John, kwa usimamizi wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha, amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, Dk. Rogers Shemwelekwa, kwa usimamizi wa masuala ya mapato, miradi na utendaji wa Halmashauri.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, magari hayo mawili yaliyopatikana kupitia mkataba wa mradi wa TACTIC yatatumika katika utekelezaji wa miradi ikiwemo ujenzi wa barabara ya Tughe–Angulcan, barabara ya Picha ya Ndege–Lulanzi pamoja na Soko la Mnarani.
Wakati huohuo, Mstahiki Meya Mawazo amezindua darasa janja katika Shule ya Sekondari Bundikani iliyopo Kibaha.
Dk. Mawazo amesema darasa hilo ni muhimu katika kusaidia sekta ya elimu kuendana na mahitaji ya dunia ya sasa, hususan katika matumizi ya teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji.
Amesema mfumo huo unaweza kusaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa walimu kwa kuwezesha mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi wengi kwa wakati mmoja.
Katika hafla hiyo, Dk. Mawazo amemtuza kwa tuzo ya heshima Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kibaha, Dk. Rogers Shemwelekwa, kwa kutambua mchango wake katika upatikanaji wa darasa janja katika shule hiyo.





























































































































































































































































