Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amezindua Kituo cha Huduma kwa Wateja cha Wizara ya Mifugo na Uvuvi, hatua inayolenga kuimarisha mawasiliano kati ya Wizara na wadau wa sekta hizo pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Uzinduzi huo umefanyika leo, Agosti 5, 2026, katika banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ridhiwani amesema kuanzishwa kwa kituo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuboresha huduma kwa wananchi kupitia matumizi ya mifumo ya kisasa ya mawasiliano.
Amesema mfumo huo utawawezesha wafugaji, wavuvi na wadau wengine kupata taarifa sahihi kwa wakati, huku ukiwapa nafasi ya kuwasilisha maswali, maoni, ushauri na malalamiko yao moja kwa moja kwa Wizara.




“Mfumo huu utamwezesha afisa anayepokea taarifa kutoa majibu sahihi kwa wakati au kumuunganisha mdau kwa mtaalamu husika ili changamoto yake ipatiwe ufumbuzi kwa haraka,” amesema Ridhiwani.
Amesema kituo hicho pia kitasaidia Wizara kufuatilia changamoto zinazowasilishwa na kuhakikisha zinashughulikiwa kwa haraka na wataalamu husika.
Ridhiwani amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuboresha mawasiliano kati ya taasisi za umma na wananchi kwa lengo la kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma.
Ameeleza kuwa mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa taarifa na kuimarisha mawasiliano kati ya wataalamu wa Serikali na wadau wa sekta za mifugo na uvuvi.
Aidha, ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuanzisha kituo hicho, akisema ni hatua inayokwenda sambamba na jitihada za Serikali za kusogeza huduma karibu na wananchi na kuhakikisha changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.


Amewahimiza wananchi, hususan wafugaji, wavuvi na wadau wengine wa sekta hizo, kutumia kituo hicho kuwasilisha changamoto, maoni na mapendekezo ili Serikali iweze kuendelea kuboresha huduma.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani, amesema kuanzishwa kwa kituo hicho ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa wakati na huduma bora kutoka taasisi za Serikali.
Amesema Wizara imejipanga kuhakikisha kila changamoto inayowasilishwa kupitia kituo hicho inafanyiwa kazi kwa wakati na kwa weledi, ili kuongeza ufanisi wa huduma na kupunguza hasara zinazoweza kujitokeza kutokana na ucheleweshaji wa utatuzi wa changamoto.
Kamani amesema kuanzishwa kwa kituo hicho, chenye namba ya Huduma 0737476937, ni mwanzo wa maboresho zaidi katika utoaji wa huduma kwa wadau wa sekta za mifugo na uvuvi.
Ameongeza kuwa Wizara itaendelea kuimarisha mifumo yake ya mawasiliano kwa lengo la kuwafikia wadau wengi zaidi na kuhakikisha wanapata huduma zenye ubora, ufanisi na kwa wakati.






























































































































































































































































