Katika Mkutano wa 48 wa Kamati ya Urithi wa Dunia wa UNESCO unaoendelea mjini Busan, Jamhuri ya Korea, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kundi la Afrika katika Kamati ya Urithi wa Dunia kwa kipindi cha miaka miwili.
Sambamba na nafasi hiyo muhimu, Tanzania pia imechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Urithi wa Dunia, hatua inayoiweka nchi katika nafasi ya juu ya uongozi wa mfumo wa maamuzi wa Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972.
Uchaguzi huu unaakisi imani kubwa ambayo nchi za Afrika zimeiweka kwa Tanzania kutokana na mchango wake katika kujenga maridhiano, kuimarisha mshikamano wa bara na kutetea uhifadhi na usimamizi endelevu wa maeneo ya Urithi wa Dunia. Aidha, ni uthibitisho wa nafasi inayozidi kuimarika ya Tanzania katika diplomasia ya kimataifa na ushiriki wake wenye tija ndani ya UNESCO.
Kupitia uongozi huu, Tanzania itaratibu misimamo ya Kundi la Afrika katika masuala yanayohusu urithi wa dunia, kuongoza majadiliano ya bara, na kushirikiana kwa karibu na Kituo cha Urithi wa Dunia, Taasisi za Ushauri na wadau mbalimbali katika kuhakikisha maslahi ya Afrika yanaendelezwa na maeneo yake ya urithi yanahifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Uchaguzi huu ni heshima kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ushahidi wa kuendelea kuaminiwa kwake katika uongozi wa masuala ya kimataifa, hususan katika sekta ya utamaduni, urithi na ushirikiano wa kimataifa.





























































































































































































































































