Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ametembelea banda la Kilombero Sugar mjini Morogoro wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki yaliyofanyika mkoani humo.
Katika ziara hiyo, Waziri Kapinga alipatiwa taarifa kuhusu uwekezaji wa kimkakati unaofanywa na Kilombero Sugar, ikiwemo kiwanda kipya cha kisasa cha K4 ambacho sasa kimeanza kufanya kazi rasmi.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kiwanda hicho kinachangia kuongeza uzalishaji wa sukari nchini na kuendeleza jitihada za Tanzania kuelekea kujitosheleza kwa sukari.
Aidha, Waziri Kapinga alipatiwa taarifa kuhusu chapa ya bidhaa ya Kilombero Sugar, Bwana Sukari. Taarifa hiyo iliwasilishwa na Meneja wa Mawasiliano na Mahusiano kwa Wadau wa Kilombero Sugar, Victor Byemelwa.
Kilombero Sugar imeeleza kuwa itaendelea kujizatiti katika kuchochea ukuaji endelevu kupitia uwekezaji wa kimkakati na ushirikiano madhubuti na wadau mbalimbali.





























































































































































































































































