Wakulima wa mahindi nchini Tanzania wametakiwa kuhakikisha wanahakiki mbegu kabla ya kuzipanda ili kujikinga na mbegu bandia na zisizokidhi viwango, ambazo zinaweza kupunguza mavuno na kuwasababishia hasara kubwa.
Wito huo umetolewa jijini Mwanza Jumanne, wakati wakulima, wafanyabiashara wa mbegu na wadau wa kilimo walipokusanyika kushuhudia uzinduzi wa kampeni ya kitaifa inayolenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kununua na kupanda mbegu za mahindi zilizothibitishwa.
Wakulima wamehimizwa kuhakikisha kuwa mbegu wanazonunua zimehakikiwa na kuthibitishwa na Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), ambayo ndiyo mamlaka ya kitaifa yenye jukumu la kusimamia ubora wa mbegu na kuhakikisha kuwa mbegu zinazouzwa kwa wakulima zinakidhi viwango vilivyowekwa.
Kampeni hiyo ya kitaifa ya miezi minne, inayojulikana kama “DEKALB Mafanikio Shambani,” inalenga wakulima wa mahindi kote nchini Tanzania, ikichanganya elimu kuhusu uhakiki wa mbegu na kuongeza uelewa wa aina mbalimbali za mbegu chotara zilizothibitishwa na zinazofaa kwa mazingira tofauti ya uzalishaji.
Kampeni hiyo inalenga aina tano za mbegu chotara za mahindi za DEKALB zilizotengenezwa kwa ajili ya maeneo tofauti ya kiikolojia, yakiwemo maeneo yenye mvua chache na yale yenye uwezo mkubwa wa uzalishaji. Aina hizo zinalenga kuwapa wakulima chaguo la mbegu zinazofaa mazingira yao ya uzalishaji, hususan wakati huu ambapo mabadiliko ya mifumo ya mvua na changamoto nyingine za tabianchi vinaendelea kuathiri uzalishaji wa kilimo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bayer Life Science Tanzania, Mwinyi Sango, alisema mabadiliko ya tabianchi yameongeza shinikizo kwa wakulima wadogo, hali inayofanya uchaguzi wa mbegu bora na zinazofaa mazingira husika kuwa muhimu zaidi katika kuongeza tija ya kilimo.
“Wakulima wadogo ndio wanaobeba athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa isiyotabirika barani Afrika. Kama taasisi inayotambua usalama wa chakula kuwa sehemu ya usalama wa taifa, tunahamasisha matumizi ya mbegu zilizothibitishwa ambazo zinaweza kuwasaidia wakulima kuongeza mavuno huku zikichangia kilimo endelevu,” alisema Sango.
Kampeni hiyo inakuja wakati mahindi yakiwa zao linaloongoza katika mfumo rasmi wa mbegu nchini Tanzania. Kwa mujibu wa TOSCI, mahindi yalichangia takribani asilimia 93 ya mbegu zote zilizothibitishwa zilizopatikana nchini katika mwaka wa 2025/26, jambo linalodhihirisha umuhimu wa zao hilo katika sekta ya mbegu na katika kuhakikisha usalama wa chakula nchini.
Kwa upande wa wakulima, Sango alisema uwezo wa mbegu kuota, usafi wake wa kinasaba na kufaa kwa aina husika katika mazingira fulani ya uzalishaji ndivyo vinavyoamua kama uwekezaji unaofanywa wakati wa kupanda utaleta mazao yenye tija.
“Huhitaji kupanda mbegu nyingi za mahindi kwenye shimo moja ili tu uwe na uhakika kuwa kitu kitaota. Unachohitaji ni mbegu moja bora, ipandwe kwa usahihi, na tunakuhakikishia itaota,” alisema.
Takwimu za TOSCI zinaonyesha kuwa mfumo rasmi wa mbegu unachangia takribani asilimia 40 ya mbegu zinazotumika nchini, wakati asilimia 45 zinakadiriwa kutoka kwenye mfumo usio rasmi na asilimia 15 nyingine zikitokana na mfumo wa Mbegu Zilizotangazwa Ubora, yaani Quality Declared Seed (QDS).
Mwakilishi wa TOSCI katika hafla hiyo ya Mwanza aliwataka wakulima kununua mbegu kutoka kwa wafanyabiashara walioidhinishwa na kuhakikisha kuwa mbegu hizo zimethibitishwa kabla ya kupandwa, akionya kuwa matumizi ya mbegu bandia au zisizokidhi viwango yanaweza kumsababishia mkulima hasara ambazo mara nyingi huonekana baada ya kutumia fedha nyingi katika maandalizi na usimamizi wa shamba.
“Wakulima wanapaswa kufanya uhakiki wa mbegu kuwa sehemu ya kila ununuzi wanaoufanya. Nunua mbegu kutoka kwa wafanyabiashara walioidhinishwa, hakikisha mbegu imethibitishwa ipasavyo na usipande mbegu ambayo huwezi kuthibitisha ubora na chanzo chake. Mbegu duni inapopandwa, mkulima anaweza kupoteza gharama ya mbegu pamoja na fedha, nguvu kazi na muda aliowekeza katika msimu mzima wa kilimo,” alisema mwakilishi huyo.
Kwa Bayer, kampeni hiyo inalenga kuifikisha moja kwa moja kwa wakulima elimu kuhusu umuhimu wa mbegu bora, huku ikiwapa motisha ya kuhakikisha wanahakiki mbegu wanazonunua.
Katika kipindi cha miezi minne ya kampeni, wakulima watakaoshiriki watakuwa na nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali, zikiwemo pampu za kunyunyizia dawa za mgongoni, simu janja, mashine za kupandia mahindi zinazoendeshwa kwa mkono, pikipiki, paneli za sola na mashine za kukoboa mahindi. Wakulima wawili pia watajishindia magari mawili aina ya Toyota pick-up.
“Tunawasaidia wakulima kulinda mavuno yao kwa kuhakikisha wanahakiki mbegu halisi kabla ya kupanda, huku tukitoa motisha inayosaidia kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa mbegu bora na usalama wa chakula,” alisema Sango.
Katika kipindi cha kampeni hiyo, Bayer itatumia fursa hiyo kuwafikia wakulima kwa elimu kuhusu mbegu bora pamoja na suluhisho nyingine za kilimo zinazolenga kusaidia uzalishaji endelevu wa chakula nchini.


















































































































































































































































































