• August 7, 2026
  • Mwandishi Wetu
  • 1

NGORONGORO: Wawakilishi wa jamii ya Kimaasai kutoka Tarafa za Ngorongoro, Loliondo na Sale wameiomba Serikali kusitisha mchakato wanaodai unahusu mabadiliko ya umiliki wa ardhi za vijiji vyao, wakisema hatua hiyo inaweza kuathiri haki za ardhi na ustawi wa wananchi.

Katika tamko walilolitoa kwa vyombo vya habari, wawakilishi hao wamesema mwezi Juni 2026, Ofisi ya Msajili wa Hati za Ardhi iliagiza baadhi ya vijiji vya Loliondo, ikiwemo Ololosokwan, Soitsambu, Enguserosambu na Arash, kuwasilisha hati za usajili wa ardhi kwa ajili ya zoezi lililoelezwa kuwa ni marekebisho ya usajili.

Wamesema wana wasiwasi kuhusu mchakato huo, wakidai unaweza kusababisha mabadiliko katika umiliki wa ardhi za vijiji bila ushirikishwaji wa wananchi wa maeneo husika.

Kwa mujibu wa tamko hilo, wawakilishi hao wameeleza kuwa vijiji hivyo vilisajiliwa kwa kuzingatia taratibu za kisheria, hivyo wameitaka Serikali kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu lengo na hatua za zoezi hilo.

Kuhusu Tume ya Rais ya Ardhi, wamesisitiza umuhimu wa taarifa ya tume hiyo kuwekwa wazi kwa wananchi ili waweze kuifahamu na kuelewa mapendekezo au maelekezo yaliyotolewa.

Wamesema masuala ya ardhi yanapaswa kuendeshwa kwa uwazi na kuzingatia ushirikishwaji wa wananchi wanaoishi katika maeneo husika.

Katika eneo la uhifadhi, wawakilishi hao wameeleza wasiwasi wao kuhusu mpango wa kuanzisha eneo la usimamizi wa wanyamapori (Wildlife Management Area – WMA) katika eneo la Ziwa Natron, wakisema utekelezaji wake unapaswa kuzingatia maslahi ya wananchi wa vijiji vinavyohusika.

Aidha, wameitaka Serikali kuendelea kuboresha huduma za kijamii katika Tarafa ya Ngorongoro, hususan elimu, afya na maji, wakieleza kuwa huduma hizo ni muhimu katika kuimarisha maendeleo na ustawi wa jamii.

Wamesisitiza kuwa jamii ya Kimaasai imekuwa ikishiriki katika uhifadhi wa mazingira kwa vizazi vingi, hivyo mipango ya uhifadhi inapaswa kwenda sambamba na ulinzi wa haki za wananchi na ushirikishwaji wao katika maamuzi kuhusu matumizi ya ardhi.

Pia wametoa wito kwa UNESCO, taasisi za haki za binadamu na wadau wa maendeleo kufuatilia utekelezaji wa sera za uhifadhi nchini ili kuhakikisha zinaendana na misingi ya haki za binadamu, utawala wa sheria na ushirikishwaji wa jamii.

1 comment on “Wamaasai Ngorongoro waiomba serikali kusitisha mabadiliko umiliki wa ardhi za vijiji”

  1. Serikali irudishe Baraza la Wafugaji Tarafa ya Ngorongoro ili liweze Kuwahudumia Wenyeji Wa Tarafa ya Ngorongoro Wananchi Wapewe Miradi Za Maendeleo Ambazo ni Afya,Maji,Barabarani na Ukarabati wa Majengo ya Shule na vituo Vya Afya Serikali Kumtumia Isack Lekisongo Meijo Kwa Maswala yote yanayohusu Ngorongoro Ngorongoro ina Wasemaji Wake Wa Kutosha Kabisa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *