Wakuu wa Wilaya za Tabora, Upendo Wella, na Kigoma, Dk. Rashid Chuachua, wameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa usimamizi mzuri wa huduma za nishati na maji nchini.
Viongozi hao walitoa pongezi hizo walipotembelea banda la EWURA katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Ipuli, Tabora, Agosti 2, 2026.




Wametoa wito kwa EWURA kuongeza hamasa kwa wananchi ili kubadili mtazamo na kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, kwa lengo la kufanikisha azma ya kufikia asilimia 80 ya watumiaji wa nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.
Aidha, viongozi hao wameisisitiza EWURA kuendelea kuhamasisha uwekezaji wa vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini, wakieleza kuwa huduma hiyo inahitajika kutokana na kukua kwa shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi.
Meneja wa EWURA Kanda ya Magharibi, Mha. Karim Ally, alitumia fursa hiyo kueleza nafasi ya EWURA katika kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa wasambazaji wakubwa wa gesi ya mitungi (LPG) katika Kanda ya Magharibi, inayohudumia mikoa ya Tabora, Shinyanga, Katavi na Kigoma.
Ally amesema kwa sasa kuna wasambazaji 19 pekee wa gesi hiyo katika eneo hilo.






























































































































































































































































