• September 18, 2026
  • Mwandishi Wetu
  • 0

Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), litaendesha uchunguzi wa bure wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu pamoja na kutoa elimu ya afya kwa abiria wanaosafiri kwa treni ya SGR kuanzia Septemba 21 hadi 29, 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Machibya Shiwa, amesema zoezi hilo ni sehemu ya shughuli za kuadhimisha Siku ya Moyo Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka Septemba 29.

Amesema katika kipindi hicho, abiria watakaosafiri kwa SGR watapata huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu pamoja na magonjwa mengine yasiyoambukiza wakiwa ndani ya treni.

Shiwa amesema SGR ni jukwaa muhimu la kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja, hivyo ushirikiano huo utasaidia kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, hususan wanaosafiri katika njia ya Dar es Salaam-Dodoma.

Amesema mpango huo unalenga kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kinga, uchunguzi wa mapema na kupata matibabu kwa wakati, huku pia ukiimarisha ushirikiano kati ya TRC na JKCI.

“Mpango huu utaimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizi mbili na kuwawezesha abiria kupata elimu ya afya wakiwa safarini,” amesema Shiwa.

Ameongeza kuwa mpango huo ni sehemu ya juhudi za taasisi za umma kutumia miundombinu na mitandao iliyopo kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, amesema taasisi hiyo itatoa wataalamu wa afya kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi na elimu kwa abiria.

Amesema mpango huo ni huduma ya mkoba inayolenga kuwafikia wananchi kupitia huduma ya SGR, ambapo wataalamu watatoa elimu kuhusu kinga, uchunguzi wa mapema na umuhimu wa kupata huduma za afya pindi mtu anapobaini dalili au changamoto za kiafya.

Dk. Kisenge amesema ushirikiano huo utaiwezesha JKCI kuwafikia watu ambao huenda wasipate fursa ya kukutana na wataalamu wa afya mara kwa mara katika vituo vya kawaida vya kutolea huduma.

Amesema awamu ya kwanza ya mpango huo itawahusisha abiria wanaosafiri kati ya Dar es Salaam na Dodoma, huku TRC ikitoa jukwaa la kufanikisha huduma hizo.

Ushirikiano huo unaongeza huduma za afya ndani ya safari za SGR, huku ukiipa JKCI njia nyingine ya kuwafikia wananchi kwa elimu na uchunguzi wa magonjwa ya moyo na yasiyoambukiza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *