Wazazi na walezi nchini wametakiwa kushirikiana kwa karibu na walimu katika kuwajengea watoto misingi ya maadili, nidhamu na imani ili kuwaandaa kuwa kizazi chenye mchango chanya katika jamii na taifa.

Rai hiyo imetolewa na Meneja wa Huduma na Mahusiano wa Benki ya CRDB Mkoa wa Pwani, Yasenta Fugara, wakati akizungumza na wazazi na walezi katika Mahafali ya 11 ya Shule za Taasisi ya EMI.

Fugara amesema ushirikiano wa wazazi na walimu ni muhimu katika kufuatilia maendeleo ya watoto, hasa katika maadili na nidhamu, ili kuwaepusha na makundi ya uhalifu na mienendo inayoweza kuathiri maisha yao ya baadaye.

Mkurugenzi wa Taasisi ya EMI, Rabo Thobias, amewataka wazazi kufuatilia maendeleo ya watoto wao na kushirikiana na uongozi wa shule kurekebisha changamoto mapema kabla hazijaleta athari.

Pia amewataka wazazi kulipa ada kwa wakati ili kuiwezesha taasisi kutekeleza mipango yake ya utoaji wa elimu bora inayokwenda sambamba na malezi na nidhamu.

Mmoja wa wazazi, Anna Emil, amepongeza uongozi wa EMI kwa kutoa elimu na malezi, huku akitoa wito wa kuendelea kuwekeza katika walimu na walezi ili kuongeza ufanisi katika malezi ya wanafunzi.

Katika mahafali hayo, wanafunzi 25 walihitimu elimu ya msingi, 25 walihitimu elimu ya sekondari na 23 walihitimu chekechea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *