Dar es Salaam, Tanzania – 12 Octoba 2026 – Afrika ina idadi kubwa ya vijana duniani, ikiwa na zaidi ya vijana milioni 400 wenye umri kati ya miaka 15 na 35. Kizazi hiki kina uwezo mkubwa wa kuchangia katika kuleta maendeleo na kuamua mustakabali wa Bara la Afrika. Hata hivyo, bado kuna mamilioni ya watoto ambao wanaishi katika maeneo ambayo ugonjwa wa malaria umeenea, na maambukizi ya malaria yanayojirudia yanaendelea kuvuruga maisha yao ya utotoni na kuathiri baadhi ya hatua muhimu za ukuaji.
Taarifa kutoka kwenye tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa ugonjwa wa malaria huwaathiri watoto chini ya miaka mitano nchini Tanzania kwa kiwango kikubwa, hali inayoonesha kuwa watoto wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa huo. Wakati mwingine, vimelea wa malaria jamii ya Plasmodium falciparum humshambulia binadamu kwa pamoja na jamii nyingine za vimelea vya malaria.
Wataalamu wanatoa angalizo kuhusu athari za ugonjwa wa malaria katika maisha ya watoto na kusisitiza suala hili kupewa kipaumbele zaidi.
“Malaria haiathiri tu afya ya mtu kwa wakati ule anapougua. Ugonjwa wa Malaria huathiri matukio ya kipindi cha utotoni, mwendelezo wa kujifunza, utulivu wa familia, pamoja na fursa za vijana kutumia na kufikia kikamilifu uwezo wao.” anasema Dk. Brian Tarimo, Mwanasayansi Kiongozi, Mradi wa Transmission Zero (T0), katika Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI). “Mustakabali wa baadaye wa Afrika utajengwa na vijana wanaokua leo. Kila mtoto anastahili kupata fursa ya kujifunza, kukua na kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya jamii yake bila kukumbwa na madhara ya magonjwa ya mara kwa mara yanayoweza kuzuilika, kama vile ugonjwa wa malaria.”
Kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2025 kuhusu ugonjwa wa Malaria, watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanaendelea kuwa miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa zaidi ya kupata ugonjwa wa malaria barani Afrika. Familia nyingi zenye watu wanaougua mara kwa mara katika miaka ya mwanzoni ya umri wao, hukumbwa na changamoto mbalimbali za kimwili, kihisia pamoja na kiuchumi.

“Katika jamii nyingi, ugonjwa wa malaria si ugonjwa unaotokea mara moja tu. Watoto wanaweza kuugua mara kadhaa ndani ya mwaka mmoja” Anasema Dk. Tarimo. “Hali hii inapotokea mara kwa mara, huathiri familia nzima, walezi, shule na jamii.”
Dk. Tarimo anasisitiza kuwa kufanya tafiti kwenye afua za nyongeza za kuzuia malaria ni muhimu kwa ajili ya afya na ustawi wa vijana na kunapaswa kuendelea kuwa sehemu ya msingi ya vipaumbele vya maendeleo ya Bara la Afrika.
Nchini Tanzania, Taasisi kama vile Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kwa kushirikiana na washirika wa kimataifa; Imperial College London, na Swiss Tropical and Public Health Institute zinafanya kazi kwa pamoja katika kuendeleza ubunifu wa teknolojia ya kichocheojeni (gene drive) kwa lengo la kuboresha matokeo ya muda mrefu ya afya kwa watoto na familia kwa ujumla. Juhudi hizi zinafanyika kupitia Programu ya Transmission Zero. Katika utafiti wetu, kichocheojeni ni zana inayowezesha sifa mahususi za kijenetiki kurithishwa kwa kiwango kikubwa zaidi kwenye mbu. Kwa kufanya jamii ya mbu wanaosambaza malaria kuwa na kinga dhidi ya ugonjwa huo, tunaweza kuzuia kwa kiasi kikubwa maambukizi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya mbu.
Tafiti zote zinazoendelea kwa sasa zinafanyika katika mazingira ya maabara yenye udhibiti madhubuti nchini Tanzania na unalenga mbu jamii ya Anofelesi.
“Barani Afrika, watu wengi wanaishi katika maeneo yaliyo katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa malaria, na asilimia 94 ya matukio yanayohusu ugonjwa wa malaria duniani huripotiwa kutoka Afrika. Kuwalinda watoto dhidi ya ugonjwa wa malaria leo ni hatua muhimu ya kulinda mustakabali wao wa baadaye na hatimaye, uwezo wa kizazi kijacho cha Afrika.”










































































































































































































































































