• August 6, 2026
  • Mwandishi Wetu
  • 0


MWANZA:
 Mahakama ya Mwanzo Mkuyuni, Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, imemhukumu kifungo cha nje cha miezi sita Elizabeth Chacha Mugusuhi (30) baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili katika Kesi ya Jinai Namba 1012/2026.

Elizabeth, ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Butimba jijini Mwanza, amepandishwa kizimbani leo Agosti 6, 2026, katika mahakama hiyo na kuhukumiwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mkuyuni, John Mgonya.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mgonya amesema mahakama imezingatia kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na hakusumbua mahakama baada ya kukiri makosa yaliyokuwa yakimkabili.

Amesema kwa kuzingatia mazingira hayo, mahakama imeona kumpa adhabu ya kifungo cha nje cha miezi sita ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kifungu cha 2(1)(a) cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu, Sura ya 11, Nyongeza ya III, Marejeo ya mwaka 2023.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, mshtakiwa atatakiwa kufanya kazi za jamii kwa kipindi chote cha kifungo chake, na endapo atakiuka masharti hayo, adhabu hiyo itabadilika na kuwa kifungo cha ndani.

Awali, akisoma hati ya mashtaka, Mwendesha Mashtaka, Sajenti Doroth Mauma, aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo akifahamu kuwa ni kinyume cha sheria.

Amesema Julai 25, 2026 majira ya saa 8:00 usiku katika eneo la Kituo cha Polisi Nyegezi, mshtakiwa alitoa taarifa za uongo kwa Mkuu wa Kituo hicho akidai kuwa ametekwa na watu wasiojulikana, huku akijua kuwa taarifa hiyo si ya kweli.

“Pia siku hiyo hiyo majira ya saa 8:00 usiku, ulijipatia kiasi cha Sh800,000 kwa njia ya udanganyifu baada ya kuomba fedha hizo kwa madai kuwa umetekwa,” amesema Doroth.

Baada ya kusomewa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili, Elizabeth alikiri kutenda makosa hayo na kuiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na ana watoto wadogo wanaomtegemea.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kosa la kwanza lilikuwa kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma kinyume na Kifungu cha 122(a) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2023.

Kosa la pili lilikuwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kinyume na Kifungu cha 302 cha sheria hiyo hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *