• August 3, 2026
  • Mwandishi Wetu
  • 0

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Musa Omar, ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa mafanikio ya kusajili mbegu za malisho, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha uzalishaji wa mifugo na kupunguza migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Balozi Omar alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la TALIRI katika Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya John Samwel Malecela, jijini Dodoma.

Akiwa katika banda hilo, alipata fursa ya kujionea huduma na teknolojia mbalimbali zinazozalishwa na taasisi hiyo, zikiwemo mbari bora za mifugo, malisho na mbegu za malisho, pamoja na teknolojia za utengenezaji wa vyakula vya ziada vya mifugo.

Aidha, Waziri huyo ameipongeza TALIRI kwa kuendelea kufanya utafiti na kubuni teknolojia zinazolenga kuongeza tija, uzalishaji na kipato cha wafugaji nchini.

“Nimeona mafanikio makubwa katika eneo la malisho. Kwa mfano, malisho ya Juncao yana uwezo wa kuzalisha hadi tani 60 kwa ekari moja. Hii ni hatua kubwa itakayosaidia kuongeza upatikanaji wa malisho na kupunguza migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi,” amesema Balozi Omar.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Prof. Erick V. Komba, amesema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza mpango wa kuwawezesha wadau mbalimbali kuzalisha mbegu za malisho, huku TALIRI ikiendelea kuwa mzalishaji wa mbegu mama ili kuhakikisha ubora wa mbegu unazingatiwa.

Prof. Komba amesema TALIRI pia imeongeza uwekezaji katika uzalishaji wa teknolojia mbalimbali za mifugo, ikiwemo kupanua maeneo ya uzalishaji wa malisho, kuongeza uzalishaji wa mbegu za malisho na kuzalisha idadi kubwa zaidi ya mifugo bora kwa ajili ya kusambazwa kwa wafugaji nchini.

Ameongeza kuwa juhudi hizo zinalenga kuongeza tija katika uzalishaji wa mifugo, kuboresha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha wafugaji na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya mifugo.

Akihitimisha, Prof. Komba amewakaribisha wafugaji, wawekezaji na wananchi kutembelea banda la TALIRI katika Maonesho ya Nanenane ili kujifunza kuhusu teknolojia mbalimbali za kisasa zinazotolewa na taasisi hiyo, kupata ushauri wa kitaalamu na kujionea fursa zilizopo katika maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *