Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amewaonya Wanaharakati, Wanasiasa na Wananchi ambao wanachochea vurugu nchini kwa kuhamasisha wananchi kuandamana na kuvuruga amani ya nchi kuacha mara moja kwani serikali haitasita kuwachukuria shieri.
Akizungumza katika ziara yake wilayani Igunga na Nzega mkiani Tabora, ya kukagua na kuweka jiwe la msingi katika Kituo cha Afya Kining’inila kinachojengwa kwa zaidi ya Sh milioni 250 na kukagua daraja la Nyandekwa lenye urefu wa mita 25.5, ambalo limefikia asilimia 98 ya ujenzi baada ya kugharimu Sh milioni 203.8.
Huku wilayani Nzega, Waziri huyo amekagua na kuweka mawe ya msingi katika nyumba mbili za watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Nzega pamoja na mradi wa mabweni, madarasa sita na matundu 10 ya vyoo katika Shule ya Sekondari Puge, kabla ya kufanya mkutano wa hadhara na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kulinda amani.
Waziri Kikwete amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika sekta za afya, kilimo na huduma za jamii ili kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza thamani ya jasho la wakulima.
Pia amewataka wakulima wa pamba wa Igunga na Nzega kuwa wavumilivu kutokana na bei ya sasa ya Sh 1,280 kwa kilo, akieleza kuwa changamoto hiyo inatokana na hali ya soko la dunia na kwamba serikali inaendelea kutafuta suluhisho la kupata bei bora, huku akiwataka wananchi kutoshawishiwa na wanaharakati nchini kuvunja amani ya nchi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Igunga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Tukai, amewataka wananchi kuendelea kuitunza amani ili kulinda miradi ya maendeleo, huku Mbunge wa Manonga, Abubakar Ally Omar, akiwahimiza wachimbaji wa madini wa Imalilo kuwa watulivu wakati serikali ikishughulikia mgogoro wao na mwekezaji.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Iyogelo wamesema ujenzi wa Kituo cha Afya Kining’inila utamaliza adha ya wajawazito kujifungulia njiani na kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya. Pia wameiomba serikali kuharakisha upatikanaji wa maji safi na salama ili kuboresha huduma katika kituo hicho na maisha ya wananchi.
Ziara ya siku tatu ya Waziri Ridhiwani Kikwete mkoani Tabora inahusisha ukaguzi na uwekaji wa mawe ya msingi katika miradi 10 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.223 pamoja na mikutano ya hadhara ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika wilaya za Igunga, Nzega, Sikonge, Tabora, Uyui, Urambo na Kaliua.





























































































































































































































































