• May 10, 2024
  • Mwandishi Wetu
  • 0

Madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kushirikiana na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanya upasuaji wa kuziba matundu ya moyo kwa watoto watatu kutoka nchini Burundi.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni ya kihistoria kwa kuwa ni mara ya kwanza kwa BMH kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka nje ya Tanzania, ikiwa ni ishara ya kuimarika kwa huduma za kibingwa nchini.

Akizungumza baada ya matibabu hayo, Dk. Ahmed Toure, bingwa wa upasuaji wa kuziba matundu ya moyo kwa watoto, amesema watoto hao walikuwa na matatizo ya kuzaliwa ya muundo wa moyo yaliyohitaji matibabu maalumu ili moyo uweze kufanya kazi vizuri. Amesema baadhi ya watoto huzaliwa wakiwa na changamoto za mishipa ya moyo hali inayoweza kusababisha madhara makubwa endapo hawatapata matibabu kwa wakati.

Dk. Toure amesema watoto wanaopata matibabu mapema huwa na nafasi kubwa ya kuendelea kuishi maisha marefu na yenye afya. Amesema watoto hao waliopatiwa upasuaji wanaendelea vizuri na wananchi wanapaswa kuendelea kuwaombea ili waendelee kupata nafuu zaidi.

Aidha, amesema ushirikiano kati ya BMH na JKCI umeonyesha umuhimu wa taasisi za afya kufanya kazi kwa pamoja katika kutoa huduma bora za kibingwa. Amesema kwa kushirikiana, wataalamu wanaweza kuongeza uwezo wa kutoa huduma za kiwango cha juu kwa wananchi wa Tanzania na nchi nyingine.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Profesa Abel Makubi, amesema ni jambo la kufurahisha kuona Tanzania ikiwa na uwezo wa kutoa matibabu ya kibingwa ambayo hapo awali wananchi walilazimika kuyatafuta nje ya nchi. Amesema ushirikiano huo utaendelea kuimarishwa ili kusaidia kukuza tiba utalii nchini.

Dk. Asha Mahita, Mratibu wa Tiba Utalii Tanzania, amesema huduma hiyo inaonyesha kuwa Tanzania inaendelea kujenga uwezo wa kutoa matibabu ya ubingwa bobezi kwa kiwango cha kimataifa. Amesema kuwahudumia wagonjwa kutoka Burundi ni hatua muhimu katika kuimarisha mahusiano na sekta ya afya kati ya nchi hizo mbili.

Naye Dk. Godwin Godfrey kutoka JKCI amesema ushirikiano huo umewapa wataalamu nafasi ya kuongeza uzoefu na kusaidia wagonjwa wengi zaidi kupata huduma karibu na maeneo yao. Amesema taasisi za afya zinapaswa kuendelea kushirikiana ili kuboresha huduma kwa wananchi.

Kwa upande wa Burundi, Dk. Nzitunga Aimee Jean kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Gitega, amesema wamefurahi kuona Tanzania ikiweza kutoa huduma hizo kwa watoto wao. Ameshukuru madaktari na uongozi wa BMH kwa kuwapatia wagonjwa matibabu salama, huku mzazi wa mtoto aliyefanyiwa upasuaji, Shedrack Nzigiyimana, akisema ana furaha kutokana na maendeleo ya afya ya mtoto wake baada ya matibabu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *