• June 27, 2024
  • Mwandishi Wetu
  • 0

Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imesema Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 uliacha majeraha kwa sehemu ya jamii kutokana na migawanyiko, vurugu na upotevu wa maisha, ikisisitiza kuwa taifa linahitaji kujenga maridhiano, haki na umoja ili kuimarisha amani ya kudumu.

Akifungua Mkutano wa 60 wa Halmashauri Kuu ya CCT pamoja na uzinduzi wa jengo la kitega uchumi jijini Dodoma, Mwenyekiti wa CCT, Askofu Stanley Hotay, amesema Kanisa lina wajibu wa kuwa sauti ya upatanisho kwa kuponya majeraha yaliyojitokeza na kuhimiza mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Amesema Kanisa haliwezi kufumbia macho yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi kwa kuwa lina jukumu la kuhubiri amani, kujenga madaraja ya mazungumzo na kuhimiza haki, ukweli na maridhiano.

“Kama Kanisa, hatuwezi kufumbia macho hali hiyo. Tunao wajibu wa kuendelea kuhubiri upatanisho, kuponya majeraha ya jamii, kujenga madaraja ya mazungumzo na kuhimiza haki, ukweli na maridhiano,” amesema Askofu Hotay.

Amesisitiza kuwa amani ya kudumu haiwezi kujengwa kwa nguvu bali kwa kuheshimu haki, ushirikishwaji wa wananchi na kuheshimiana miongoni mwa makundi yote ya jamii.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili vijana, Askofu Hotay amesema bado wanakumbwa na ukosefu wa ajira, kuporomoka kwa maadili, matumizi mabaya ya teknolojia, uraibu wa dawa za kulevya na kukata tamaa kuhusu maisha yao ya baadaye.

Kutokana na hali hiyo, amesema Kanisa linapaswa kuwekeza zaidi katika malezi ya vijana kupitia elimu ya maadili, stadi za maisha na programu za kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.

Pia amesema kupungua kwa misaada kutoka mataifa ya Ulaya na Marekani kwa nchi za Afrika kunapaswa kuwa chachu kwa makanisa kujenga uwezo wa kujitegemea kupitia uwekezaji katika miradi ya kiuchumi.

Ameeleza kuwa CCT tayari imeanza kutekeleza mkakati huo kwa kuanzisha vitega uchumi katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayolenga kuongeza mapato ya jumuiya na kuimarisha utoaji wa huduma kwa jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *