• June 27, 2024
  • Mwandishi Wetu
  • 0

Mapambano dhidi ya wadudu na magonjwa yanayoendelea kupunguza uzalishaji wa korosho nchini yameongezeka mkoani Morogoro, ambapo maafisa ugani wa kilimo wanapatiwa mafunzo ya kisasa yatakayowawezesha kuwafikishia wakulima elimu bora ya uzalishaji, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kufikia lengo la taifa la kuzalisha tani milioni moja za korosho.

Mafunzo hayo, yanayoendeshwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), yameanza katika wilaya za Mvomero na Ulanga na yanawakutanisha maafisa kilimo wa ngazi ya kata ili kuimarisha uwezo wao wa kukabiliana na changamoto zinazokwamisha uzalishaji wa zao hilo.

Washiriki wanapatiwa mafunzo na wataalamu kutoka CBT, Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Mtwara (MATI), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Kituo cha Naliendele pamoja na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA).

Mafunzo hayo yanajikita katika mbinu za kudhibiti wadudu na magonjwa yanayoweza kusababisha upotevu wa hadi asilimia 70 ya mavuno ya korosho, pamoja na matumizi sahihi ya mbegu bora, usimamizi wa mashamba na matumizi salama ya viuatilifu.

Mkufunzi kutoka MATI Mtwara, Joseph Mkude, amesema mafanikio ya jitihada hizo yatategemea uwezo wa maafisa ugani kuwafikia wakulima kwa wakati na kuwapatia elimu sahihi kuhusu kanuni bora za kilimo cha korosho.

“Mafunzo haya yatawawezesha maafisa ugani kuwa mabalozi wa teknolojia za kisasa kwa wakulima, hatua ambayo itasaidia kuongeza uzalishaji na ubora wa korosho,” amesema.

Kwa upande wake, mtafiti kutoka TARI Naliendele, George Lucas, amesema taasisi hiyo inaendelea kufanya tafiti za kuboresha teknolojia za uzalishaji wa korosho zinazokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuibuka kwa wadudu na magonjwa mapya.

Naye Afisa Kilimo wa Bodi ya Korosho Tanzania, Tawi la Morogoro, Edson Mbande, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha maafisa kilimo wa vijiji, kata na wilaya wanakuwa na uelewa wa kutosha wa kuwasaidia wakulima kuongeza tija na ubora wa zao la korosho.

Kwa upande wake, Afisa Kilimo kutoka TPHPA, Kaizer Kaluwa, amesisitiza umuhimu wa kutumia viuatilifu vinavyopendekezwa kitaalamu pamoja na kuandaa mashamba kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ili kupunguza athari za wadudu na magonjwa.

Naye Afisa Kilimo wa Kata ya Mlali, Amanda Hilary, amesema elimu aliyoipata itawasaidia kuwafikia wakulima kupitia mafunzo ya mashambani na ziara za ugani, hatua itakayochochea ongezeko la uzalishaji wa korosho katika mkoa huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *