• June 27, 2024
  • Mwandishi Wetu
  • 0

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua mfumo mpya wa kidijitali unaoitwa ‘Kilinganisha Bei’ (Price Comparison Tool) utakaowawezesha wananchi kulinganisha gharama za huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi mbalimbali kabla ya kufanya uamuzi wa kukopa au kutumia huduma za benki.

Mfumo huo unalenga kuongeza uwazi katika sekta ya fedha, kuwasaidia wananchi kuchagua huduma zenye gharama nafuu na masharti yanayowafaa, pamoja na kuchochea ushindani miongoni mwa taasisi za fedha.

Akizungumza kuhusu mfumo huo, Mchambuzi wa Masuala ya Fedha kutoka Idara ya Kumlinda Mtumiaji wa Huduma za Kifedha ya BoT, Fanuel Kijoji, amesema mtumiaji anaweza kuchagua benki moja au kulinganisha huduma zinazotolewa na benki zote ili kuona tofauti za riba, tozo na gharama nyingine kabla ya kufanya uamuzi.

“Kupitia mfumo wa Kilinganisha Bei, mwananchi anaweza kufanya uamuzi sahihi kwa kuchagua huduma ya kifedha yenye gharama nafuu na inayokidhi mahitaji yake. Mfumo huu pia unachochea ushindani miongoni mwa taasisi za fedha, jambo linaloweza kusaidia kupunguza gharama za huduma kwa wananchi,” amesema Kijoji.

Amesema mfumo huo umeanzishwa wakati ambapo wananchi wengi bado wanakabiliwa na changamoto ya kupata taarifa sahihi kuhusu gharama za huduma za kifedha, hali inayowafanya baadhi yao kukopa kwa masharti yasiyowafaa, kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati na wakati mwingine kupoteza mali zao.

Kwa mujibu wa Kijoji, hatua ya kwanza ya mfumo huo inahusisha huduma za benki, huku BoT ikipanga kuupanua ili ujumuishwe pia huduma zinazotolewa na taasisi za fedha ndogo pamoja na watoa huduma za malipo.

Ameeleza kuwa mpango huo unaunga mkono juhudi za kuongeza ushirikishwaji wa wananchi katika matumizi ya huduma rasmi za kifedha kwa kuwapa taarifa sahihi zinazowawezesha kufanya maamuzi yenye tija.

“Gharama kubwa za huduma za kifedha pamoja na ukosefu wa taarifa kuhusu huduma zilizopo ni miongoni mwa sababu zinazowazuia baadhi ya wananchi kutumia huduma rasmi za kifedha. Kupitia mfumo huu, mtumiaji anaweza kuona huduma mbalimbali zilizopo sokoni na kulinganisha gharama zake kwa urahisi,” amesema.

Kijoji amewataka wananchi kufanya utafiti na kulinganisha gharama za mikopo kabla ya kuchukua mkopo, badala ya kuangalia kiwango cha riba pekee.

“Watu wengi huangalia riba pekee na kusahau gharama nyingine zinazohusiana na mkopo. Ni muhimu kutumia mfumo wa Kilinganisha Bei kubaini taasisi inayotoa mkopo kwa masharti nafuu na ambayo mtu anaweza kuyamudu,” amesema.

Ameonya kuwa kushindwa kufanya ulinganisho wa huduma kabla ya kukopa kunaweza kusababisha wakopaji kushindwa kulipa mikopo kwa wakati, kutozwa adhabu mbalimbali na hata kupoteza mali zao, ilhali wangeweza kupata huduma nafuu zaidi kutoka taasisi nyingine kama wangepata taarifa mapema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *