Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 pamoja na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum), litakalofanyika Agosti 5 na 6, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo umebeba kaulimbiu, “Miaka Kumi ya Mafanikio: Kutoka Maono hadi Utekelezaji – A Decade of Economic Impact: From Ambition to Delivery.”
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na Mwenyekiti wa hafla ya ufunguzi wa mkutano huo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amesema maandalizi ya mkutano huo yanaendelea vizuri, huku zaidi ya washiriki 1,200 kutoka ndani na nje ya Afrika wakitarajiwa kuhudhuria.




Amesema washiriki hao wanatarajiwa kujumuisha viongozi wa Serikali, taasisi za fedha za kimataifa, wawekezaji, wawakilishi wa sekta binafsi na wadau wa maendeleo.
Balozi Omar amesema mkutano huo unafanyika katika kipindi muhimu ambapo Africa50 inatimiza miaka 10 tangu kuanza rasmi shughuli zake mwaka 2016. Africa50 ilianzishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali za Afrika na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa lengo la kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu barani Afrika.
Amesema tangu Tanzania ilipojiunga rasmi na Africa50 tarehe 14 Februari 2023 kama mwanahisa wa kundi la nchi za Afrika (African Sovereign States), nchi imenufaika kwa kupanua fursa za kushiriki katika maandalizi, uendelezaji na ufadhili wa miradi mikubwa ya miundombinu.
“Tangu Tanzania imejiunga rasmi na Africa50 tarehe 14 Februari 2023 kama mwanahisa wa kundi la nchi za Afrika (African Sovereign States) imenufaika zaidi, hatua iliyopanua fursa za nchi kushiriki kikamilifu katika maandalizi, uendelezaji na ufadhili wa miradi mikubwa ya miundombinu,” amesema Balozi Omar.
Ametaja baadhi ya miradi ambayo tayari imeanza kufanyiwa kazi kwa ushirikiano na Africa50 kuwa ni pamoja na maendeleo ya Bandari ya Mangapwani Zanzibar, Mradi wa Mini Liquefied Natural Gas (Mini LNG), miradi ya miundombinu ya usafirishaji wa umeme pamoja na upanuzi wa huduma za afya, hususan matibabu ya kusafisha figo (dialysis), kupitia Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).

Balozi Omar amesema katika siku mbili za mkutano huo kutakuwa na Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50, Jukwaa la Miundombinu Afrika pamoja na hafla za kusaini makubaliano mbalimbali ya maandalizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya miundombinu.
Amesisitiza kuwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni fursa muhimu ya kujitangaza kimataifa kama kitovu cha uwekezaji wa miundombinu katika ukanda wa Afrika Mashariki, sambamba na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za fedha za kimataifa.
“Mkutano huu unatarajiwa kuchochea biashara, kuimarisha utalii wa mikutano (MICE), kuongeza ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na mataifa mbalimbali,” amesema.
Aidha, Balozi Omar ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na kuwakaribisha wageni watakaohudhuria mkutano huo wa kimataifa.
Amesema mkutano huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa matukio makubwa ya kimataifa yatakayofanyika nchini mwaka 2026 na kutoa jukwaa muhimu la kuendeleza ajenda ya maendeleo ya miundombinu barani Afrika.


















































































