Washiriki kutoka Tanzania wanaohudhuria Mkutano wa 63 wa Shirikisho la Kimataifa la Polisi Wanawake (IAWP) nchini Indonesia wameahidi kutumia kikamilifu maarifa na uzoefu watakaoupata katika mkutano huo kwa lengo la kuboresha huduma wanazozitoa kwa wananchi nchini Tanzania.

Akizungumza mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Eda Mkisi amesema Jeshi la Polisi pamoja na washiriki wengine kutoka Tanzania wamejipanga kujifunza kutoka kwa mataifa mbalimbali yanayoshiriki mkutano huo ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Amesema mkutano huo umefungua fursa kubwa ya kukutana na wataalamu na wawakilishi kutoka nchi mbalimbali duniani, jambo ambalo litawawezesha kujifunza mbinu na uzoefu mbalimbali unaoweza kutumika kuboresha huduma za Jeshi la Polisi nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Mariam Kobero, amesema sekta ya utalii kama moja ya vyanzo muhimu vya mapato ya fedha za kigeni nchini Tanzania huku akiweka wazi kuwa kwa umuhimu huo wataendelea kupata mafunzo ndani na nje ili kuboresha huduma za uhifadhi nchini Tanzania.

Aidha amesema kuwa ushiriki wao katika mkutano huo umelenga kupata elimu na uzoefu utakaosaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, hususan katika eneo la uhifadhi.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kupata mbinu mpya ambazo zinaweza kutumika kuboresha shughuli za uhifadhi na kuhakikisha wageni wanaotembelea maeneo ya hifadhi wanapata huduma bora.

Naye Wakili wa Serikali, (Adv) Fortunata Shija, amesema ushiriki katika mkutano huo utawasaidia kuongeza ujuzi na umahiri katika kutafsiri na kusimamia sheria nchini Tanzania.

Amesema maarifa na uzoefu watakaoupata kutoka kwa washiriki wa mataifa mbalimbali vitakuwa na mchango katika utekelezaji wa majukumu yao baada ya kurejea nchini.

Kwa upande mwingine, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Edith Mbogo amesema ana furaha kushiriki katika mafunzo hayo, akieleza kuwa anatarajia kutumia maarifa yatakayopatikana kuboresha huduma za urekebishaji katika Jeshi la Magereza nchini Tanzania.

Amesema uzoefu kutoka nchi mbalimbali utawasaidia kupata mitazamo na mbinu mpya katika kutekeleza majukumu yao.

Naibu Kamishna wa uhamiaji DCI Bahati Mwaifuge kutoka idara ya uhamiaji akaweka wazi kuwa mafunzo hayo yatachangia kuboresha huduma zinazotolewa kwa wageni wanaoingia nchini Tanzania pamoja na wananchi kwa ujumla huku akisistiza kuchota mbinu mpya ya kutoa huduma za kiuhamiaji.

Wamesema kupitia uzoefu watakaoupata kutoka kwa nchi mbalimbali, wataweza kuboresha zaidi namna ya kuwahudumia wageni na wananchi, huku wakizingatia weledi na viwango vya huduma vinavyokubalika kimataifa.

Mkutano wa 63 wa IAWP unaofanyika jijini Bali, Indonesia, umewakutanisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali duniani kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu ya ulinzi, usalama, utekelezaji wa sheria na utoaji wa huduma kwa jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *