MOROGORO – Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani limeanzisha operesheni maalumu ya kukamata na kukagua magari ya shule ambayo hayakuitikia wito wa kufanyiwa ukaguzi wa hiari kipindi cha likizo, huku magari 15 yakizuiwa kuendelea kutoa huduma baada ya kubainika kuwa na kasoro za kiusalama.
Akizungumza wakati wa operesheni hiyo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Morogoro, SSP Gabriel Chiguma, alisema Jeshi la Polisi lilitoa muda wa kutosha kwa shule zote kupeleka magari yao kwa ukaguzi wa hiari kabla ya kuanza kwa muhula mpya wa masomo.
Alisema taarifa kuhusu ukaguzi huo ziliwasilishwa kwa shule husika kupitia barua rasmi pamoja na ujumbe katika makundi ya mawasiliano, lakini mwitikio ulikuwa mdogo hali iliyosababisha Jeshi hilo kuanza operesheni ya kuyatafuta na kuyakagua magari hayo kwa lazima.
“Shule nyingi hazikuitikia wito tulioutoa, hivyo tumelazimika kufanya operesheni hii kuhakikisha hakuna gari lisilokaguliwa linaloendelea kubeba wanafunzi. Lengo letu ni kulinda maisha ya watoto,” alisema SSP Chiguma.
Alisema katika operesheni hiyo, jumla ya magari 25 yalikaguliwa, ambapo 15 yalizuiwa baada ya kubainika kuwa na hitilafu mbalimbali ikiwemo matatizo ya mifumo ya injini na breki, uchakavu wa magari pamoja na kutokidhi matakwa ya kisheria kuhusu alama na rangi za magari ya shule.
Kwa mujibu wa SSP Chiguma, magari hayo hayataruhusiwa kurejea barabarani hadi yatakapofanyiwa marekebisho, kukaguliwa tena na kuthibitishwa kuwa yanakidhi viwango vya usalama.
Alisema magari 10 yaliyokaguliwa yalikutwa yakiwa katika hali nzuri na kuruhusiwa kuendelea na shughuli za usafirishaji wa wanafunzi.
Aidha, amepiga marufuku matumizi ya magari binafsi ya kukodi kwa ajili ya kusafirisha wanafunzi, akisema hayana sifa za kisheria na yanaweza kuhatarisha usalama wa watoto.
Aliwataka wazazi kuepuka kuchangia huduma za usafiri zisizo rasmi na kuhakikisha watoto wao wanatumia magari ya shule yanayotambulika na kukaguliwa kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, dereva wa gari la shule, Tompson Patrick, alisema ukaguzi huo una umuhimu mkubwa kwa wamiliki wa magari na madereva kwa kuwa husaidia kubaini mapema hitilafu zinazoweza kuhatarisha maisha ya wanafunzi.
Naye mzazi wa mwanafunzi, Devota, alisema hatua hiyo imeongeza imani kwa wazazi kuhusu usalama wa watoto wao wanapotumia usafiri wa shule, huku akiomba operesheni hiyo iendelee kufanyika mara kwa mara.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limesema operesheni hiyo itaendelea katika maeneo mbalimbali kuhakikisha magari yote yanayosafirisha wanafunzi yanakaguliwa na kuzingatia viwango vya usalama barabarani.





























































































































































































































































