Bweni la wanafunzi wa kiume katika Shule ya Sekondari Kalangalala, mkoani Geita, limenusurika kuteketea baada ya moto kuzuka mchana wa leo na kusababisha taharuki miongoni mwa wanafunzi, walimu na wananchi.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Kenneth Mwakasitu, tukio hilo lilitokea majira ya saa sita na dakika 16 mchana. Alisema moto huo ulizimwa kwa haraka na wanafunzi kwa kushirikiana na walimu kabla haujasambaa na kusababisha uharibifu mkubwa.
Mwakasitu alisema mafanikio ya kuudhibiti moto huo yametokana na elimu ya kujikinga na kukabiliana na majanga ya moto ambayo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limekuwa likitoa katika shule mbalimbali.


Aliongeza kuwa uchunguzi umeanza kubaini chanzo cha moto huo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Hadi sasa hakuna taarifa za vifo au majeruhi zilizoripotiwa, ingawa baadhi ya mali zilizokuwa ndani ya bweni hilo zimeharibika kutokana na moto.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kalangalala, Antideus Deusidenti, pamoja na mwanafunzi wa Kidato cha Tatu, Yusuf Antony, walisema hatua za haraka zilichukuliwa mara baada ya moto kuzuka, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa, kuwahamisha wanafunzi na kushiriki kuuzima moto kabla haujasambaa katika sehemu nyingine za bweni.
Mamlaka zimewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu huku wakisubiri matokeo ya uchunguzi yatakayobaini chanzo cha moto huo na kiwango halisi cha uharibifu uliosababishwa.































































































































































































































































