Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Rhimo Nyansaho, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Mahmoud Thabit Kombo, wamefanya mazungumzo na ujumbe maalumu wa wajumbe 11 wa Baraza la Wawakilishi la Marekani (Congress), kutoka vyama viwili vikuu vya nchi hiyo.
Ujumbe huo uliongozwa na Ronny Jackson, Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Huduma za Kijeshi, Ulinzi na Usalama ya Baraza la Wawakilishi la Marekani (House Armed Services Subcommittee).
Mazungumzo hayo yaliyofanyika hivi karibuni katika Ofisi za Makao Makuu ya zamani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Ngome Upanga, Dar es Salaam, yalilenga kujadili maeneo ya kipaumbele katika uhusiano kati ya Tanzania na Marekani.


Maeneo hayo ni pamoja na biashara, uwekezaji, ulinzi na usalama, pamoja na hali ya amani na usalama katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Katika mazungumzo hayo, pande hizo zilionyesha dhamira ya kupanua ushirikiano wa biashara na uwekezaji, hususan katika sekta za kimkakati zikiwemo gesi asilia (LNG), madini muhimu, usafiri wa anga, ulinzi na usalama.
Aidha, Tanzania ilisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano kati ya wananchi wa nchi hizo mbili kwa kuondoa vikwazo vya visa kwa Watanzania wanaosafiri kwenda Marekani, pamoja na vikwazo vingine vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Tanzania.

Kwa upande wake, ujumbe wa Marekani uliipongeza Tanzania kwa mchango wake katika kudumisha amani na usalama wa kikanda, ikiwemo juhudi za kupambana na ugaidi na ushiriki wake katika operesheni za kulinda amani barani Afrika.
Pande hizo mbili zilikubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika maeneo yenye maslahi ya pamoja.
Aidha, zilikubaliana kupitia upya maombi yote ya kuondolewa kwa vikwazo yaliyowasilishwa rasmi na Tanzania na kuendelea na mawasiliano katika vikao vijavyo kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo.
Kikao hicho kimeelezwa kuwa hatua muhimu ya awali katika kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Marekani.































































































































































































































































