• August 6, 2026
  • Mwandishi Wetu
  • 0

Kampuni ya Vitol Bahrain E.C., kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Uganda National Oil Company (UNOC), zimeingia makubaliano ya kuendeleza mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta ghafi (refinery) jijini Tanga wenye thamani ya takribani Dola za Marekani bilioni 20 (zaidi ya Shilingi trilioni 56 za Kitanzania), hatua inayotarajiwa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha nishati na biashara ya mafuta Afrika Mashariki.

Hati ya Makubaliano (MoU) kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Tanga Regional Energy Hub imesainiwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam mbele ya Marais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda.

Mbali na ujenzi wa refinery, mradi huo pia unahusisha ujenzi wa bohari la kuhifadhi na kupakia mafuta yaliyosafishwa (terminal tank farm), eneo maalumu la kupokelea mafuta bandarini (jetty) pamoja na bomba la kusafirisha mafuta yaliyosafishwa kutoka Tanga kwenda Uganda (pipeline).

Mradi huo utahakikisha Tanzania na Uganda zinanufaika na mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya mafuta (full value chain), ambapo mafuta ghafi kutoka Uganda yatasafirishwa hadi Tanga kwa ajili ya kusafishwa kabla ya kusambazwa nchini Tanzania, Uganda na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza thamani ya sekta ya mafuta, kuvutia uwekezaji mkubwa zaidi, kuongeza ajira, kukuza shughuli za Bandari ya Tanga na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara ya mafuta na nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *