Tanzania na Belarus zimekubaliana kuanzisha ushirikiano wa kitaaluma kati ya taasisi za elimu ya juu, utakaowezesha kubadilishana wataalamu, kufanya tafiti za pamoja na kupanua fursa za ufadhili wa masomo kwa vijana wa kitanzania nchini Belarus.
Hatua hiyo imejadiliwa baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, kutembelea Chuo Kikuu cha Belarusian State na kufanya mazungumzo na uongozi wa chuo hicho kuhusu namna ya kuanzisha ushirikiano na taasisi za elimu ya juu nchini Tanzania.
Ziara hiyo ilifanyika Agosti 5, 2026, wakati Prof. Mkenda akiwa nchini Belarus kwa ziara ya kikazi kufuatia mwaliko wa Waziri wa Elimu wa nchi hiyo, Andrei Ivanets.

Prof. Mkenda amesema Chuo Kikuu cha Belarusian State ni miongoni mwa vyuo vikuu vinavyotambulika kimataifa na vinavyovutia wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali, yakiwemo China, Urusi, Afrika Kusini, Zimbabwe na Cameroon.
Akiwa katika Ofisi za Wizara ya Elimu ya Belarus, Prof. Mkenda amesema Tanzania ina nia ya kuona vijana wengi zaidi wanapata nafasi ya kusoma nchini humo, hususan katika vyuo vinavyobobea katika sayansi na teknolojia.
“Ushirikiano huu utasaidia kuongeza fursa za masomo, kubadilishana uzoefu wa kitaaluma na kuimarisha maendeleo ya rasilimali watu kupitia elimu, sayansi na teknolojia,” amesema Prof. Mkenda.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu wa Belarus, Andrei Ivanets, ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, akibainisha kuwa mwaka 2025 Tanzania na Belarus zilisaini makubaliano ya ushirikiano katika sekta za elimu, sayansi na teknolojia.
Ivanets amesema Serikali ya Belarus itaanza mara moja mchakato wa kuwezesha vijana wa Tanzania kupata fursa zaidi za masomo katika vyuo vya nchi hiyo, hususan kozi zitakazopendekezwa kulingana na mahitaji ya taifa ya wataalamu na ujuzi.


































































































































































































































































