Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Wahusika wa Ghasia na Ukiukwaji wa Sheria katika matukio ya ghasia wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 imeanza rasmi kazi ya kuchunguza kwa kina wahusika na matukio yaliyoibua vifo, majeruhi, watu kupotea na uharibifu wa mali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 24, 2026, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Shaban Ally Lila, amesema Tume imeundwa kufuatia mapendekezo ya Tume ya awali iliyoongozwa na Jaji Joseph Chande, iliyochunguza ghasia zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi huo.
Amesema Tume mpya inalenga kubaini wahusika wa ghasia hizo na namna walivyoshiriki katika kupanga, kufadhili, kuratibu au kutekeleza vitendo vya ghasia.
Tume hiyo ina Makamishna sita, akiwamo Jaji Lila kama Mwenyekiti, pamoja na Petrus Tileinge Damaseb wa Namibia, Barishaki Bonny Cheborion wa Uganda, na Majaji Wastaafu wa Tanzania Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishiel Nelson Sumari. Katibu wa Tume ni Paul Kadushi.
Yafichuliwa maeneo ya uchunguzi
Kwa mujibu wa Jaji Lila, Tume itachunguza pia matukio yaliyotokana na hatua za kudhibiti ghasia, ikiwemo madai ya vifo visivyo vya kawaida vya watoto na watu wa makundi maalum.
Aidha, itachunguza madai ya watu kujeruhiwa kwa kutumia silaha za moto kinyume cha sheria, watu kupigwa risasi nje ya maeneo ya ghasia pamoja na taarifa za watu waliopotea wakati na baada ya uchaguzi.
Tume pia itachunguza madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi kinyume na sheria, taratibu na miongozo wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Jaji Lila amesema Tume itatumia ushahidi wa moja kwa moja, nyaraka pamoja na kutembelea maeneo yaliyohusika katika matukio hayo ili kupata taarifa sahihi na za kina.
Amesisitiza kuwa Tume itazingatia haki ya kusikilizwa, ikiwamo kuwapa nafasi watu wote watakaoguswa na taarifa zitakazowasilishwa ili kutoa maelezo yao.
Tume ina siku 150
Tume imepewa siku 150 kuanzia tarehe ya uzinduzi kukamilisha uchunguzi na kuwasilisha taarifa yake.
Jaji Lila amewataka wananchi wenye taarifa zinazohusiana na Hadidu Rejea za Tume kujitokeza na kuwasilisha taarifa hizo ili kusaidia uchunguzi.
Amesema Tume imeamua kukutana na waandishi wa habari ili kuwafahamisha wananchi kuwa imeanza kazi na kuwaomba vyombo vya habari kushirikiana nayo katika kuwahamasisha wananchi kutoa taarifa muhimu.





























































































































































































































































