Wananchi wa Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma, wameeleza namna Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ilivyowasaidia kupata ushauri na huduma za kisheria katika kutatua changamoto zao.
Amina Abedi Mbawala, mkazi wa Namtumbo, amesema amepata msaada wa kisheria kuhusu madai ya mirathi ya baba yake, ikiwemo ushauri na msaada wa kuandaa nyaraka muhimu bila gharama.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kampeni hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Juma Zuberi Homera amewataka wananchi wenye changamoto za kisheria kujitokeza kunufaika na huduma hizo.
Amesema huduma hizo zinahusisha masuala ya mirathi, ndoa, talaka, madai, migogoro ya ardhi, pamoja na upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa na vifo.
Dk. Homera amesema Wizara, kwa kushirikiana na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali, imeweka timu Namtumbo kwa ajili ya kuwafikishia wananchi huduma hizo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za Serikali kwa urahisi na kwa wakati.































































































































































































































































