Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetembelea na kukagua miundombinu mbalimbali ya maji, ikiwemo mabomba makuu ya usambazaji maji, kwa lengo la kuchukua tahadhari na maandalizi kuelekea mvua za El Nino zinazotarajiwa kuanza kunyesha kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba mwaka huu.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi DAWASA, Mhandisi Romanus Mwangingo, amesema Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imetoa utabiri wa kuwepo kwa mvua za El Nino na tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Muheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekwisha toa maelekezo kwa taasisi za serikali kuchukua tahadhari mapema.


“Leo tumetembelea miundombinu ya maji kujionea hatua za haraka zinazotakiwa kuchukuliwa, ikiwemo ukarabati wa miundombinu ya zamani na kuelekeza Menejimenti ya DAWASA kuleta mpango wa tahadhari kuelekea mvua za El Nino,” amesema Mhandisi Mwangingo.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, amesema Mamlaka tayari imeanza kutekeleza hatua mbalimbali za maandalizi, ikiwemo ununuzi wa dawa za kutibu maji kwa wingi na ukarabati wa miundombinu inayohusisha mabomba makuu ya usambazaji maji.
“Leo tumefika katika eneo la Mpiji ambapo kuna mabomba makuu mawili ya usafirishaji maji ya inchi 54 na 72 ambayo yana historia ya kusombwa na mvua hivyo tumefika kuona hatua za tahadhari zinazoweza kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa na ufanisi na kuwezesha upatikanaji wa huduma ya maji kwa uhakika kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani wakati wa mvua hizo” alisema Mhandisi Bwire
Hatua hizo ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo, hususan athari zinazoweza kuathiri miundombinu ya maji na uzalishaji wa maji, huku Mamlaka ikiendelea kusisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari mapema.































































































































































































































































