Wilaya ya Kilosa imeamua kuelekeza fedha za maafa katika ununuzi wa vifaa vya dharura na kuwaandaa wananchi wanaoishi maeneo hatarishi kukabiliana na mvua kubwa za El Nino zinazotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.
Uamuzi huo umetangazwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, wakati akiongoza kikao maalum cha Kamati ya Maafa ya Wilaya kilichowakutanisha Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na wadau mbalimbali kujadili maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua hizo.
Shaka amesema Wilaya ya Kilosa imejifunza kutokana na mafuriko yaliyotokea miaka ya nyuma, hivyo maandalizi ya safari hii yatajikita katika hatua za vitendo badala ya mipango kubaki kwenye nyaraka.

Amesema fedha zilizotengwa kwa ajili ya maafa zinapaswa kutumika kununua vifaa vinavyohitajika wakati wa dharura, ikiwemo boti za uokoaji, mablanketi na dawa.
“Wilaya ya Kilosa tumeamua fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya maafa zitanunua vifaa vya dharura vinavyoonekana. Wananchi wa Kilosa wanajua mafuriko ni nini. Wanachohitaji ni boti la kuwaokoa, blanketi la kujifunika na dawa wakiumwa,” amesema.
Amesema maandalizi hayo yanatekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kutaka mikoa na wilaya kuchukua tahadhari mapema na kuhakikisha taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zinafuatiwa kwa kuchukua hatua za vitendo.
Katika hatua nyingine, kikao hicho kimeazimia kuanzishwa kwa Stoo ya Dharura ya Wilaya kwa ajili ya kuhifadhi vifaa vitakavyohitajika wakati wa maafa, pamoja na kuhamisha wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi.
Wadau walioshiriki kikao hicho wamepongeza ushirikishwaji wa makundi mbalimbali katika maandalizi hayo, wakisema mipango iliyowekwa inalenga kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi wakati wa mvua hizo.






























































































































































































































































