• October 13, 2026
  • Mwandishi Wetu
  • 0

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) unashiriki katika Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2026 yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, kwa lengo la kutoa elimu kuhusu huduma za hifadhi ya jamii na matumizi ya mifumo ya kidijitali inayorahisisha upatikanaji wa huduma za Mfuko.

Akizungumza katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu na Utawala wa Mfuko wa PSSSF, Bw. Paul Kijazi, amesema maonesho hayo ni fursa muhimu kwa Mfuko kuwafikia wanachama na wananchi kwa ujumla, kuwapatia elimu ya hifadhi ya jamii na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kujiandaa mapema kwa maisha baada ya kustaafu.

Amesema PSSSF inaendelea kutumia majukwaa mbalimbali, ikiwemo maonesho, kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu huduma za Mfuko na maboresho mbalimbali yaliyofanywa ya mifumo na mafao.

Aidha, amesema katika maonesho hayo, PSSSF inatoa huduma na elimu kwa wanachama na wastaafu kuhusu matumizi ya mfumo wa mtandao wa PSSSF Portal unaowawezesha mwanachama na mstaafu kupata huduma mbalimbali za Mfuko kwa njia ya kidijitali.

Kupitia mfumo huo, wanachama wanaweza kupata taarifa zinazohusu michango yao, taarifa za mafao na huduma nyingine zinazopatikana mtandaoni, hatua inayosaidia kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza ulazima wa kufika ofisini kwa baadhi ya mahitaji.

Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa, pamoja na kuwajengea uelewa kuhusu fursa zinazoweza kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kijamii.

Maadhimisho ya mwaka 2026 yanaongozwa na kauli mbiu isemayo: “Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Vijana.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *