• August 18, 2022
  • Mwandishi Wetu
  • 0

Watu wawili wamefariki dunia huku wengine 50 wakiokolewa baada ya boti iliyokuwa ikisafirisha abiria kutoka Kisiwa cha Goziba kuelekea jijini Mwanza kushika moto katikati ya Ziwa Victoria usiku wa kuamkia leo, Julai 9, 2026.

Kwa mujibu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, waliofariki ni mtoto wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 10 na mwanaume mwingine mwenye umri unaokadiriwa kuzidi miaka 60.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Elisa Mugisha, amesema operesheni ya uokoaji imefanikiwa kuwaokoa watu 50 wakiwa hai, huku juhudi zikiendelea kuwatafuta watu wawili wanaodaiwa kutopatikana baada ya ajali hiyo.

Amesema tukio hilo lilitokea kati ya Kisiwa cha Lyamwenge na Kisiwa cha Bwiro wakati boti hiyo, inayodaiwa kusajiliwa kwa jina la MV Kalebezo, ikiwa safarini kuelekea Mwanza.

“Mpaka sasa tumeshaokoa watu 50 na kwa bahati mbaya watu wawili wamefariki dunia. Tunaendelea kuthibitisha idadi halisi ya abiria waliokuwemo kwenye chombo hicho na kuwatafuta wanaodaiwa kutoweka,” amesema Mugisha.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, boti hiyo ilidaiwa kuwa na abiria 52, hata hivyo Mugisha amesema jeshi hilo linaendelea kuhakiki idadi rasmi kupitia kumbukumbu za safari ili kubaini kama kuna watu wengine ambao bado hawajapatikana.

Amesema manusura wote waliokolewa wakiwa na fahamu, huku baadhi yao wakipata mshtuko na uchovu kutokana na tukio hilo na kupelekwa katika vituo vya afya kwa ajili ya matibabu na uangalizi.

“Hawakuwa na majeraha makubwa. Wengi walipata mshtuko na kuchoka kutokana na tukio, lakini wote waliokolewa walikuwa na fahamu zao,” amesema.

Mugisha amesema hali mbaya ya hewa, ikiwemo upepo mkali uliokuwa ukivuma katika Ziwa Victoria, ilichelewesha vikosi vya uokoaji kufika eneo la tukio.

“Upepo ulikuwa mkali kiasi kwamba tulilazimika kusimama kwenye kisiwa kimoja kwanza kusubiri hali itulie. Tulipofika eneo la tukio, boti ilikuwa tayari imeteketea kwa moto hivyo hatukuweza kuizima,” amesema.

Ameongeza kuwa kwa sasa kipaumbele cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ni kukamilisha operesheni ya kuwatafuta watu wanaodaiwa kutoweka kabla ya kuanza uchunguzi wa kubaini chanzo cha moto.

“Bado hatujaanza uchunguzi wa chanzo cha moto. Tutaufanya baada ya kukamilika kwa operesheni ya uokoaji,” amesema.

Jeshi hilo pia linaendelea kuhakiki taarifa za usajili wa chombo hicho, ambacho kwa mujibu wa taarifa za awali kinajulikana kwa jina la MV Kalebezo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *