Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi za Afrika zenye bei nafuu ya petroli, huku lita moja ikiuzwa kwa wastani wa Sh3,990, licha ya misukosuko inayoendelea katika soko la mafuta duniani.

Kwa mujibu wa takwimu za Global Petrol Prices zilizochapishwa na Business Insider Africa, Malawi inaongoza kwa bei ya juu zaidi ya petroli barani Afrika, ambapo lita moja inauzwa kwa takribani Sh10,135, ikifuatiwa na Rwanda Sh5,408 na Zimbabwe Sh5,211.

Nchi nyingine zenye bei kubwa ni Jamhuri ya Afrika ya Kati (Sh4,941), Shelisheli (Sh4,593), Uganda (Sh4,541), Sierra Leone (Sh4,528), Cape Verde (Sh4,506), Kenya (Sh4,439) na Senegal (Sh4,336).

Kwa bei ya Sh3,990 kwa lita, Tanzania haijaingia katika orodha ya nchi 10 zenye petroli ghali zaidi Afrika, huku Senegal ikiingia kwenye orodha hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kuiondoa Afrika Kusini.

Tofauti za bei zinaendelea kuchangiwa na sababu mbalimbali, ikiwemo kodi, gharama za usafirishaji, kushuka kwa thamani ya fedha za ndani na utegemezi wa uagizaji wa mafuta.

Ripoti hiyo pia inaonyesha wastani wa bei ya petroli duniani umeongezeka kutoka dola 1.48 hadi dola 1.49 kwa lita ndani ya mwezi mmoja.

Wachambuzi wanaonya kuwa mvutano katika njia muhimu za usafirishaji wa mafuta, hususan Mlango wa Hormuz na Bab el-Mandeb, unaweza kuongeza shinikizo la bei duniani na kuathiri zaidi nchi za Afrika zinazotegemea uagizaji wa mafuta.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *