Kamishna wa Idara ya Upelelezi wa Kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Hashim Ngoda, amekutana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, kwa lengo la kujadili mikakati ya kuimarisha mapambano dhidi ya magendo katika maeneo ya Kunduchi, Mbweni na Bagamoyo.
Viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya TRA, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na vyombo vingine vya dola ili kuziba mianya ya magendo, kulinda mapato ya Serikali na kuhakikisha sheria za nchi zinafuatwa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mtambule amesema kuanzia Daraja la Tanzanite mpaka Bagamoyo, Pangani ni miongoni mwa maeneo yanayotumiwa kupitisha bidhaa kwa njia zisizo halali, hususan mafuta ya kula kutoka Zanzibar yanayoingia nchini bila kufuata taratibu za kisheria.
Ameeleza kuwa bidhaa zinazoingizwa kwa njia hizo ni vigumu kuthibitisha ubora na usalama wake.



















































































































































































































































































