Katika kutekeleza falsafa ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya ‘Kazi na Utu’, Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Ashatu Kijaji amelielekeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), kufanya upya uthamini wa eneo la familia 13 zilizoondolewa katika maeneo yao kupisha uanzishwaji wa Hifadhi ya Taifa ya Ibanda – Kyerwa ili walipwe fidia stahiki.
Dk.Kijaji ametoa maelekezo hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Isingiro Wilayani Kyerwa Mkoani Kagera baada ya baadhi ya wananchi kuhoji ucheleweshwaji wa ulipwaji wa fidia baada ya kuondolewa katika maeneo yao kupisha shughuli za uhifadhi katika hifadhi hiyo.
Aidha, Waziri Kijaji ametaka kufanywa upya uthamini wa maeneo ya wananchi hao na kumuelekeza Kamishna Mkuu wa TANAPA,Missana Mwishawa kuanza kazi hiyo ndani ya mwezi huu wa Agosti, 2026 ili kujua thamani halisi ya maeneo ya wananchi hao baada ya kupita muda mrefu tangu uthamini wa awali kufanyika.




Katika mkutano huo wa hadhara mbali na madai hayo ya fidia pia wananchi hao wamelalamikia kasi ndogo ya mkandarasi anayejenga barabara ya Murongo hadi Omurushaka na kutaka kutafutwa kwa mkandarasi mwingine atakayejenga kwa kasi zaidi kwa kuzingatia viwango na thamani ya fedha, na kuiomba serikali kutatua kero za maji na barabara.
Akijibu hoja hizo za wananchi Dk.. Kijaji amesema inatekeleza miradi mbalimbali ya maji ya muda mfupi na mrefu katika wilaya hiyo na kuwaahidi kuwa ifikapo mwishoni mwa Desemba, mwaka huu, baadhi ya miradi itakuwa imekamilika na kupunguza adha ya ukosefu wa maji.
Awali, Dk. Kijaji akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahaya Kido, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera, Nazir Karamagi pamoja na watendaji wengine wa Serikali amekagua ujenzi wa lango la wageni katika hifadhi ya Ibada – Kyerwa wenye thamani ya Sh. bilioni 3.5 sambamba na kuweka jiwe la msingi na kuelekeza kuanza mara moja kazi ya kuitangaza hifadhi hiyo sambamba na kuboresha miundombinu hususani ya barabara ili kuwawezesha watalii kunufaika na vivutio vya utalii vilivyopo katika hifadhi hiyo.
Pia Dk. Kijaji alitembelea na kukagua Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kinachojengwa katika Kijiji cha Kagenyi, unaogharimu kiasi cha Sh. bilioni 1.8 na kutaka mradi huo utakapokamilika pamoja na fani nyingine pia liwepo somo la masuala ya utalii na ukarimu ili kuwasaidia vijana kupata ujuzi na kujikwamua kiuchumi kwa kujiajiri kutokana na fursa ya uwepo ya hifadhi hiyo ya Ibanda – Kyerwa.































































































































































































































































