Simba 10 wameuawa katika eneo la Ndutu, Kata ya Endulen, Wilaya ya Ngorongoro, katika tukio linalodaiwa kuhusishwa na kisasi baada ya wanyama hao kuwaua na kuwala punda wawili wa wafugaji.
Taarifa za awali zilieleza kuwa simba watano waliuawa jana Septemba 19, 2026, majira ya saa 4:00 asubuhi, kabla ya idadi hiyo kufikia 10.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, simba hao wanadaiwa kuuawa kwa kulishwa mzoga wenye sumu, siku mbili baada ya tukio la kuuawa kwa punda hao lililoripotiwa Septemba 17, 2026.
Jeshi la Polisi pamoja na askari wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wamefika eneo la tukio na wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha vifo hivyo na waliohusika.
Iwapo uchunguzi utathibitisha kuhusika kwa watu katika mauaji ya wanyamapori hao, hatua za kisheria zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Tukio hilo linatokea wakati Ndutu ikiripotiwa pia kukumbwa na uharibifu wa baadhi ya miundombinu ya maji, ikiwemo visima na mabomba yaliyojengwa na NCAA katika miezi ya Agosti na Septemba mwaka huu.
Tathmini ya awali imeibua madai kwamba uharibifu huo unaweza kuwa na lengo la kusababisha uhaba wa maji na kuibua mazingira ya kudai kuruhusiwa kwa mifugo kuingia katika maeneo yaliyowekewa zuio kwa sababu za uhifadhi.






























































































































































































































































