Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhammed Mussa, ameongoza ujumbe wa Tanzania kushuhudia Mashindano ya 48 ya Ujuzi Kidunia (Worldskills Competition) yanayofanyika jijini Shanghai, China tarehe 22 hadi 27 Septemba, 2026.
Waziri ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, wataalamu kutoka Wizara hizo pamoja na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Mamlaka ya Amali(VTA) Zanzibar




Tanzania imealikwa kwenye mashindano ikiwa ni mwanachama wa Worldskills Africa kwa lengo la kujifunza namna mashindano hayo yanafanyika katika ngazi ya Kimataifa na kukutana na wadau mbalimbali kubadilishana uzoefu na kuimarisha mahusiano na taasisi, makampuni na viwanda katika masuala ya uendelezaji ujuzi.
“Tumejionea namna ambavyo mashindano haya yanafanyika ngazi ya Kimataifa na hivyo tuna jukumu la kuwezesha vijana wetu kushiriki kwa wingi katika mashindano haya kwa miaka inayofuata,” amesema

Amesema ushiriki wa Tanzania kwenye tukio hilo umekuja wakati sahihi ambapo tayari Tanzania imeanza kuandaa Mashindano ya Ujuzi kwa kufuata vigezo vya Worldskills na kwamba ushiriki huo unatoa fursa kwa Tanzania kujiimarisha zaidi katika uendeshaji wa Mashindano.



































































































































































































































































